Na Joyce Kasiki,Timesmajira online


SERIKALI kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeanza kutekeleza Mpango wa Matengenezo ya Kawaida ya Barabara kwa Kushirikisha Jamii (CBRM) unaolenga kuboresha zaidi ya kilomita 15,000 za barabara nchini kasoro mkoa wa Dar Es Salaam huku ukitoa ajira kwa zaidi ya vikundi 3,000 vya wananchi katika kipindi cha miaka mitatu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 10,2026 katika banda la TARURA lililo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Mratibu wa TARURA Makao Makuu na Mshauri wa Programu ya CBRM, Mhandisi Richard Misa, alisema mpango huo unatekelezwa kupitia mradi wa Serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) kwa ufadhili wa mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Alisema utekelezaji wa programu hiyo ni wa miaka mitatu unahusisha miaka ya fedha 2025/2026 hadi 2027/2028, ukiwa na lengo la kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote kwa kufanya matengenezo ya kawaida kupitia vikundi vya wananchi vinavyoishi karibu na barabara husika.
Mhandisi Misa alifafanua kuwa shughuli zinazotekelezwa ni pamoja na kusafisha mitaro, makaravati na madaraja, kuondoa vikwazo barabarani, kupunguza vichaka kandokando ya barabara pamoja na kuziba mashimo madogo ili kuzuia uharibifu mkubwa hasa kipindi cha mvua.
Alisema utekelezaji wa awamu ya kwanza tayari umeanza katika mikoa ya Tanga, Pwani, Morogoro na Dodoma, ambapo zaidi ya kilomita 1,500 za barabara zimeanza kufanyiwa matengenezo na vikundi 82 vimenufaika kwa kupata fursa za ajira.
Aidha, alisema mpango huo unalenga kuongeza ajira na kipato cha wananchi wa maeneo ya vijijini na mijini, kujenga umiliki wa miundombinu ya barabara katika jamii na kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kwa kuhakikisha barabara zinabaki katika hali nzuri mwaka mzima.
Aliongeza kuwa vikundi vinavyopewa kazi huchaguliwa kutoka maeneo yanayozunguka barabara husika na hupewa mikataba ya muda ili viendelee pia kujishughulisha na shughuli nyingine za kiuchumi, sambamba na kupatiwa mafunzo ya ujasiriamali kwa lengo la kuviwezesha kujitegemea.
Mhandisi Misa alisema mpango huo pia unatekeleza sera ya Serikali inayotaka asilimia 30 ya bajeti za ununuzi wa umma zitengwe kwa ajili ya makundi maalumu kupitia shughuli zinazotekelezwa na wananchi, huku akisisitiza kuwa hauondoi nafasi ya wakandarasi na wakandarasi wa labor-based ambao wataendelea kushiriki katika miradi mingine ya ujenzi na matengenezo ya barabara.
Misa ametoa wito kwa vijana kuchangamikia fursa hiyo ili waweze kujiajiri na kukuza kipato chao na hivyo kuchangia katika pato la Taifa.

More Stories
Wananchi watakiwa kujenga tabia ya kufanya mazoezi
Ujuzi wa vitendo nguzo ya kujitegemea
Mahundi ahimiza ushiriki kujenga,kulinda miradi