April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania yazindua maandalizi ya Kongamano la 10 la Jotoardhi

Na Penina Malundo, timesmajira

TANZANIA imezindua maandalizi ya kuandaa Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika (ARGeo-C10) ambalo litafanyika kuanzia Novemba 11 hadi 17, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi huo umefanywa leo jijini Dar es Salaam na Kamshina wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga ambaye alisema kongamano hilo la jotoardhi litahusuisha nchi 50 zikiwemo wanachama wa ARGeo ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Ethiopia na Djibout.
Amesema katika kongamano hilo zaidi ya watu 1,000 wa kada mbalimbali zinazohusiana na sekta hiyo muhimu katika kuzalisha nishati safi na salama wanatarajiwa kushiriki.
Mhandisi Luoga amesema mwaka 2022 Rais Samia Suluhu Hassan alikubali ombi la Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kufanyika kwa kongamano hilo, hivyo kuanzia sasa Tanzania inaendelea na maandalizi ili liweze kufanyika.
Kamishna Luoga amesema kongamano hilo ni muhimu kwa Tanzania kutokana na kuwa na rasilimali nyingi za jotoardhi, hivyo matumaini yao ni kuwa washiriki wataweza kujifunza na kubadilishana taaluma.
Amesema Serikali kupitia Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) itashirikiana na UNEP kuhakikisha kongamano hilo muhimu linafanikiwa kwa kiwango kikubwa, ili dhamira ya serikali kuongeza nishati jadidifu inafikiwa.
“Novemba 11 hadi 17, 2024 Tanzania inakuwa mwenyeji wa kongamano la jotoardhi ambalo litakutanisha wataalam, wawekezaji, wafanyabiashara na viongozi mbalimbali ambao watapata nafasi ya kuchochea kasi ya uzalishaji nishati hii,” amesema.
Mhandisi Luoga amesema tafiti zilizopo zinaonesha Tanzania inaweza kuzalishaji megawati 5,000 za umeme wa jotoardhi na kwa sasa wanatekeleza miradi mbalimbali ambayo inatarajiwa kuzalisha megawati 200 ifikapo 2027, hivyo kusaidia nchi kukabiliana na changamoto ya umeme.
Amesema rasilimali ya jotoardhi ilianza kufanyiwa utafiti tangu mwaka 1970 hivyo kwa sasa wanaendelea na utekelezaji wa kuzalisha kupitia TGDC ambapo wameanza kwenye baadhi ya maeneo kati ya 51 yanayoweza kuzalisha nishati hiyo.
“Tuna maeneo matano ambayo tumeyaainisha kwa ajili ya uzalishaji wa nishati ya jotoardhi ambayo ni Ngozi tutazalisha megawani 70, Kiejo Mbaka megawati 60, , Natron megawati 60, Songwe megawati tano na Ruoyi Kisaki megawati tano, hadi kufikia megawati 200,” amesema.

Kamishna huyo amesema pamoja na kongamano hilo kukutanisha wataalam mbalimbali, pia sekta binafsi na wananchi wa kawaida watanufaika kwa siku tano za kongamano.
Amesema wamealika taasisi mbalimbali za kifedha ili ziweze kupata taarifa ya fursa ya uwepo wa jotoardhi nchi ili waweze kuwekeza.
Kwa pande wake Meneja wa TGDC, Mhandisi Mathew Mwangomba amesema kampuni kongamano hilo limekuja wakati muafaka kwa kuwa dunia ipo katika mapambano ya kupunguza hewa ukaa ambayo imekuwa na madhara makubwa katika mazingira.
Mhandisi Mwangomba amesema upatikanaji wa jotoardhi nchini unaendana na hatua tatu muhimu ambazo ni sayansi jiolojia, jiofizikia na jiokemia ambayo ipo nchini kupitia Bonde la Ufa la Magharibi, Mashariki na Kusini (Tripple Juction).

“Sisi kama TGDC tunaelekea Ngozi kuchimba nishati ya jotoardhi ambayo inapatikana kwa nyuzi joto 250, hivyo basi kukutana kwa wadau 1,000 kujadili jotoardhi tunaenda kupiga hatua zaidi,” amesema
Mwakilishi Mkazi wa UNEP Tanzania, Clara Makenya wanatarajia kongamano hilo litakuja kutoa mwanga kwa duania kuwekeza katika nishati safi na salama kama jotoardhi na kuachana na nishati ambazo zina madhara kwa jamii na mazingira.