May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania yapata mapokezi makubwa maonesho ya 68 ya Vito Thailand

Naibu Katibu Mkuu Mbibo awataka Wafanyabishara, Wachimbaji kuchangamkia fursa

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Ushiriki wa Tanzania katika Maonesho ya 68 ya Vito na Usonara katika jiji la Bangkok nchini Thailand umewavutia Wafanyabiashara mbalimbali wa madini kutokana na wengi kutumia malighafi za madini kutoka nchini.

Akizungumza baada ya kushiriki hafla fupi ya ufunguzi wa maonesho hayo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amesema wafanyabiashara wakubwa wa madini nchini humo wakiwemo viongozi wa Serikali wameonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali zikiwemo biashara ya madini, uongezaji thamani madini pamoja na kubadilishana uzoefu katika shughuli hizo.

Aidha, Mbibo amesema uwepo wa Tanzania katika maonesho hayo ya madini yenye thamani kubwa unalenga kujifunza pamoja na kuhamasisha urejeshwaji wa minada ya madini nchini na kuhamasisha uwepo wa masoko ya madini ambapo wafanyabiashara hao wanaweza kununua madini kupitia masoko ya madini yaliyoanzishwa katika kila mkoa nchini.

Serikali kupitia Wizara ya Madini inatarajia kurejesha tena minada ya madini nchini pamoja na Maonesho ya Kimataifa ya Vito na Usonara ya Arusha yatakayofanyika kila mwaka kulingana na kalenda za kimataifa ya maonesho ya madini ya vito na biashara za usonara.

Aidha, hivi karibuni Serikali kupitia Tume ya Madini ilitoa taarifa kuwa, Wizara ipo kwenye mchakato wa kuwasilisha mapendekezo ya maboresho ya Sheria na Kanuni ili kuwezesha maonesho na minada ya vito kufanyika nchini ikiwemo marekebisho ya Kanuni za Eneo Tengefu la Mirerani za Mwaka 2021 ambazo zilizuia kuuzwa kwa madini ya Tanzanite nje ya Mirerani.

Kufuatia hayo, Mbibo ametoa wito kwa wauzaji, wachimbaji, waongezaji thamani madini kutumia uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Thailand ambao umekuwepo kwa muda mrefu kuchangamkia fursa hiyo ikiwemo kuungana na wadau wa nchi hiyo katika masuala yanayohusu mnyororo wa shughuli za madini.

Ameongeza kwamba, tayari Serikali ya Awamu ya Sita imefungua milango ya biashara katika Sekta ya Madini na kuwataka wadau wa madini nchini kutumia fursa hiyo kuwapokea wawekezaji mbalimbali ili hatimaye kujenga uchumi imara na kuinua ustawi wa watanzania kupitia rasilimali madini.

‘’Biashara lazima iwe na wauzaji na wanunuzi wawe tayari kupokea watu wengine na wajifunze namna ya kufanya biashara kutoka biashara ya kitaifa hadi kimataifa kwa madini ya thamani na mawe,’’ amesema Mbibo.

Akizungumza baada ya ujumbe wa Tanzania kutembelea banda la Kampuni ya Bright Future katika maonesho hayo, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Ashish Baid ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Madini nchini humo na mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite na madini mengine, ameelezea nia yake ya dhati kupitia jukwaa hilo na kampuni yake binafsi ya kushirikiana na Tanzania katika kuipa thamani ya kimataifa minada ya madini endapo Serikali itakuwa yatari kushirikiana nao ikiwemo katika eneo la uongezaji thamani madini.

Ameongeza kwamba, kwa kuzingatia uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Thailand na kutokana na utajiri wa rasilimali madini zilizopo nchini ikiwemo madini pekee ya Tanzanite, wananchi wa Tanzania na taifa hawana budi kunufaika ipasavyo na rasilimali hiyo na si kwa wafanyabiashara pekee wa madini na kuongeza,’ ’ikiwa sisi wafanyabiashara tunanufaika ni muhimu sana Kwa Tanzania kunufaika,” amesema.

Naye, Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Fine Gamestone Sukharit Sinchawla baada ya kutembelewa na ujumbe wa Tanzania amesema amefurahishwa na uwepo wa Tanzania katika maonesho hayo na kusema ni nchi nzuri yenye madini mengi mazuri na yenye thamani kubwa na kueleza kwamba ni nchi ambayo kampuni yake inatumia madini mengi kufanya biashara yakiwemo ya Spinel na Tanzanite.

Maonesho ya BangKok ni moja ya maonesho ya madini ya vito na usonara maarufu zaidi duniani na yamekuwepo nchini humo kwa miaka mingi. Maonesho hayo yameandaliwa na Idara ya Ukuzaji Biashara ya Kimataifa ya Thailand.

Aidha, biashara ya madini nchini humo imetajwa kuwa ya pili katika kuchangia fedha za kigeni ikiwemo kukuza ajira .

Wadau muhimu wapatao 31 elfu kutoka maeneo mbalimbali duniani wanatarajia kutembelea maonesho hayo kutoka nchi 21 na waoneshaji takribani 1,100.

Imeelezwa kuwa mwaka 2022 mauzo ya vito na usonara nchini humo yalifikia thamani ya Dola za Marekani milioni 800 na mwaka huu mauzo yanatarajiwa kufikia Dola za Marekani milioni 850.

Maonesho ya BangKok ni maonesho makubwa na ya kuaminika ambayo wafanyabiashara wachimbaji wanaweza kuyatumia kujenga uhusiano wa kibiashara, kutangaza bidhaa zao na kuuza.

Mbali na Naibu Katibu Mkuu, wengine wanaoshiriki ni wawakilishi kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Wataalam kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini.