April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania rasmi kupokea watalii kutoka kila kona ya Dunia, Bodi ya Utalii yaja na mikakati kabambe

Na Irene Clemences, TimesMajira

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt.Hamisi Andrea Kigwangalla kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) leo amezindua rasmi filamu inayoitambulisha Tanzania ndani na nje ya nchi katika maeneo mbalimbali ya utalii.

Filamu ambayo inaendana na kauli mbiu ya Tanzania Unforgettable (Tanzania isiyosahaulika) ambayo imejikita kuitambulisha Tanzania duniani kote kupitia huduma bora za kitalii na vivutio vilivyopo hapa nchini.

Dkt.Kigwangala amefanya uzinduzi huo katika makao makuu ya Bodii ya Utalii nchini yaliyopo jijini Dar es Salaam.

Amesema,Tanzania imeendelea kutangaza utalii ndani na nje ya nchi licha ya changamoto ya uwepo wa virusi vya ugonjwa wa Corona (Covid-19), kwani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli ameiongoza vyema nchi katika mapambano bila kuathiri sekta za kiuchumi ikiwemo utalii hapa nchini.

Wziri huyo amesema kuwa, Tanzania imejipanga kuwahudumia vyema watalii watakaowasili nchini na kuhakikisha kuwa wanaondoka salama ili wakifika katika nchi zao wapeleke habari njema kwamba Tanzania ni salama na watalii ambao walisita kuja waje bila woga kwa ajili ya kujionea vivutio mbalimbali.

“Kwa namna ya kipekee, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutuongoza vyema katika mapambano ya Covid-19 bila kuathiri sekta za kiuchumi ikiwemo hii ya utalii. Kwani kwa sasa tumefungua sekta hii, kama mnavyojua biashara ni ushindani atakeyewahi kufungua na kuweka misingi mizuri ya kuwahudumia wageni na wahudumu sekta ya utalii ndiye atakayepata faida zaidi, tumeamua kufungua utalii wetu na sasa anga letu lipo wazi kwa watalii,”amesema Waziri huyo.

Pia Waziri wa Maliasili na Utalii amesema,Serikali imeamua kufungua sekta ya utalii kwa kufuata tahadhari zote zinazotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Alitumia fursa hiyo kuwakaribisha watalii kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kutembelea vivutio mbalimbali nchini.

Wakati wa uzinduzi huo, Waziri huyo ametoa rai kwa Watanzania kuisambaza filamu hiyo kwenye mitandao yao ya kijamii ikiwemo Twitter, Telegram, Instargram, Facebook, blogu na mingine mingi ili iweze kuwafikia walengwa kwa lengo la kutangaza Tanzania kiutalii katika soko la utalii la kimataifa zaidi.

“Hii ni video rasmi au filamu fupi kwa lengo la kuitambulisha nchi yetu kiutalii katika soko la utalii kimataifa, na hii imeendana sawa kabisa na kauli mbiu ya
Tanzania Unforgettable kwa hiyo ninaomba Watanzania wenzangu tuisambaze kwenye mitandao yetu ya kijamii kwa maana imetafsiriwa katika lugha mbalimbali ikiwemo Kiswahili, Kingereza, Kifaransa, Kihispania, Kiisrael na Kichina,”amesema Waziri wa Maliasili na Utalii.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB),Devotha Mdachi amesema kuwa, Tanzania kwa sasa imejikita zaidi kutangaza vivutio vya utalii kupitia mitandao ya kijamii, kwa hiyo kuzinduliwa kwa filamu hiyo fupi kutawasaidia kuteka soko la ndani na nje ya nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii nchini (TTB), Devota Mdachi akimkaribisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Hamisi Andrea Kigwangalla wakati wa uzinduzi wa filamu hiyo jijini Dar es Salaam leo.

“Sisi kama Bodi ya Utalii tumejikita zaidi kutangaza utalii kwa kutumia mitandao ya kijamii, kwani mpaka sasa tuna vipindi vinavyoruka mubashara kupitia mitandao
yetu kwa mfano kipindi cha Serengeti Safari Show na kile kinachorushwa na Mamlaka ya Bonde la Ngorongoro, hizi ni moja ya njia za kutangaza utalii ndani na nje ya nchi,”amesema Mdachi.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji huyo ameongeza kuwa, kupitia filamu hiyo fupi watalii watapata fursa ya kuona utamaduni na maeneo mbalimbali ya kuvutia na kuweza kuchagua sehemu sahihi ya kwenda kutembelea.

Pia amewataka Watanzania hasa watu maarufu kusambaza filamu hizo za dakika moja, dakika tatu, dakika saba na dakika 10 kwenye kurasa zao ili ziweze kufika mbali zaidi na katika maeneo tofauti tofauti duniani.

Uzinduzi huo ni hatua mahususi na mikakati kabambe ya Bodi ya Utalii nchini kuhakikisha kuwa, Tanzania inapiga hatua kubwa kupitia sekta ya utalii ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.