
Na Moses Ng’wat, Songwe.
SERIKALI imesaini mkataba wa mradi wa kimkakati wa uchimbaji na uvunaji wa gesi ya helium baina yake na kampuni ya Helium One Global Limited kupitia Kampuni ya Ubia ya Songwe Helium Limited, hatua inayofungua njia ya kuanza uzalishaji wa rasilimali hiyo adimu duniani.
Mradi huo unatarajiwa kuanza uzalishaji rasmi Novemba 2027, na kuifanya Tanzania kuingia kwenye soko la kimataifa la helium lenye thamani kubwa huku ushindani ukiwa mdogo.
Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo ilifanyika Aprili 2, 2026 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe na kushuhudiwa na
viongozi mbalimbali wa serikali, pamoja na wawakilishi wa wananchi, wakiwemo viongozi wa dini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa, alisema Tanzania imeanza safari mpya ya kihistoria ya uzalishaji wa helium.
Alieleza kuwa mradi huo gesi ya Helium wa Southern Rukwa ni wa kimkakati na utaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa rasilimali hiyo duniani.
“Kwa sasa uzalishaji wa gesi ya helium
duniani unatawaliwa na nchi chache, hususan Marekani na Qatar, zinazochangia zaidi ya asilimia 75 ya uzalishaji wote, huku Urusi, Algeria, Canada, China na Poland zikichangia kwa kiwango kidogo” alibainisha Dk. Kiruswa.
Aliongeza kuwa mahitaji ya helium duniani yamefikia zaidi ya futi za ujazo bilioni sita kwa mwaka na yanatarajiwa kuongezeka zaidi ifikapo mwaka 2030 kutokana na matumizi yake katika sekta za teknolojia na afya.
Aidha, Dk. Kiruswa alisema Serikali itamiliki asilimia 17 ya hisa katika kampuni ya ubia ya Songwe Helium Limited ili kuhakikisha taifa linanufaika moja kwa moja na rasilimali hiyo.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Majadiliano ya Wizara ya Madini, Sifuni Mchome, alisema mfumo wa Serikali kumiliki hisa huru zisizohafifishwa thamani unaipa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika miradi ya madini.

Alisema kupitia utaratibu huo, Serikali itanufaika kwa kupata gawio, mrabaha, kodi na tozo mbalimbali huku ikihakikisha uwazi, uwajibikaji na ulinzi wa maslahi ya wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Helium One Global Limited, Lorna Blaisse, alisema mradi huo uko tayari kuanza uzalishaji wa kibiashara baada ya mafanikio ya utafiti.
Alibainisha kuwa mafanikio ya kisima cha Itambula West-1 mwaka 2024 yalithibitisha uwepo wa helium kwa kiwango kinachoweza kuendelezwa kibiashara.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omari Makame, alisema mradi huo utachochea maendeleo ya kiuchumi kwa kuongeza ajira, kuboresha miundombinu na kuinua kipato cha wananchi wa eneo hilo.



More Stories
Shule za Sekondari nane zanufaika na Kitulo Garden Maratho
TTB yaeleza Utalii wa michezo unavyochangia uchumi wa jamii
Rais Samia apongeza tuzo wafanyakazi bora ,JOWUTA yawatunza waandishi sita