Na Penina Malundo,Timesmajira
Tanzania na Brazil zimekutana katika mkutano wa siku tatu wenye lengo la kubadilishana uzoefu na mbinu za kupambana na utumikishwaji wa watoto katika sekta ya kilimo cha pamba,huku zikisisitiza umuhimu wa kazi zenye staha na ustawi wa mtoto.
Mkutano huo umeandaliwa kupitia mradi wa Promotion of Decent Work in the Cotton Value Chain in Tanzania unaoratibiwa na Shirika la Kazi Duniani(ILO),ukihusisha Serikali ya Tanzania na Brazil katika kuimarisha mazingira salama ya kazi, afya kazini pamoja na hifadhi ya jamii kwa wakulima wa pamba.
Akizungumza katika mkutano huo, Mratibu wa Miradi Kitaifa wa ILO, Glory Blasio amesema mradi huo umejikita katika kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya kazi hatarishi huku familia zikipewa mazingira bora ya kiuchumi.
“Tunapozungumzia kazi zenye staha tunamaanisha mazingira salama ya kazi, afya kazini na hifadhi ya jamii. Mama akiwa salama hata mtoto anakuwa salama,” alisema Blasio.
Ameeleza kuwa changamoto za kiuchumi zimekuwa zikisababisha baadhi ya familia kuwapeleka watoto kufanya kazi mashambani badala ya shule, jambo ambalo mradi huo unalenga kulidhibiti kupitia mifumo ya hifadhi ya jamii na elimu kwa jamii.
Kwa mujibu wake, Amesema Brazil imepiga hatua kubwa katika ukaguzi wa maeneo ya kazi, jambo ambalo Tanzania inaweza kujifunza ili kuhakikisha hata maeneo yasiyo rasmi ya kilimo yanafikiwa na huduma za ukaguzi na ulinzi wa watoto.

“Mkulima wengi wanafanya shughuli zao katika maeneo yasiyo rasmi, hivyo kupitia ushirikiano huu tunataka kuhakikisha ukaguzi unafika mbali zaidi na watoto wanakuwa salama,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Kinga ya Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini, Frank Kilimba amesema mradi huo umefika wakati muafaka katika kusaidia mapambano dhidi ya utumikishwaji wa watoto kwenye kilimo cha pamba.
Amesema bado baadhi ya wazazi wanategemea nguvu kazi ya watoto katika shughuli za kilimo badala ya kutumia mbinu za kisasa zitakazoongeza uzalishaji na kupunguza utegemezi huo.
“Wazazi wanapaswa kufikiria matumizi ya teknolojia na mbinu za kisasa za kilimo badala ya kutegemea watoto wadogo mashambani,” amesema Kilimba.
Aidha amesema mtoto anatakiwa kupewa nafasi ya kupata elimu kwani hiyo ndiyo njia bora ya kumjengea maisha ya baadaye.

“Mtoto akipata elimu anaweza kuwa mkulima bora mwenye maarifa, lakini si sahihi kumuondoa shule akiwa bado mdogo na kumuingiza kwenye kazi,” amesema.
Naye Afisa Kazi Mkoa wa Simiyu, Hadija Hensi amesema kupitia mradi huo, elimu imeendelea kutolewa kwa wakulima katika Wilaya ya Meatu ili kuzuia watoto kushiriki katika hatua mbalimbali za uzalishaji wa pamba ikiwemo kupanda, kuvuna na kusafirisha mazao.
Amesema watoto wanaotumikishwa hukosa haki zao za msingi kama elimu, afya na muda wa kupumzika.
“Tumekuwa tukifanya uelimishaji mkubwa kwa jamii kuhusu madhara ya utumikishwaji wa watoto na umuhimu wa kuwapeleka shule,kwani miaka ya nyuma hali ilikuwa mbaya zaidi kuliko sasa na sababu kuu ya kufanya hivyo wazazi ukiwauliza wanasema hali ya kiuchumi,” alisema Hadija.
Aliongeza kuwa Serikali kupitia mifumo mbalimbali ikiwemo TASAF na mkakati wa taifa wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto imeendelea kusaidia kaya maskini na kuimarisha ulinzi wa watoto nchini.
Pia amesema sheria mbalimbali zimewekwa kulinda haki za watoto, ikiwemo Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 pamoja na Sheria ya Mahusiano na Ajira Kazini iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023 inayokataza watoto walio chini ya miaka 14 kufanya kazi.
“Si sawa kuwatumikisha watoto chini ya miaka 14 kwa sababu unawanyima haki zao za msingi ikiwemo elimu,” amesema.
Mradi huo sasa umefikia tamati, huku wadau wakisisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi zilizoanzishwa ili kuhakikisha watoto wanapata ustawi bora na taifa linakuwa na kizazi salama chenye elimu.

More Stories
Wizara ya Mambo ya Nje yasikitishwa na upotoshaji Hotuba ya Bajeti 2026/2027
Tuzo za waandishi wa habari kuhamasisha elimu ya hali ya hewa, yatangazwa rasmi
Serikali kujenga vituo 10 vya Gesi ya CNG