April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANESCO yawahimiza wananchi kutumia fursa za uwepo wa umeme

Na Mwandishi Wetu, Nyakabindi

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limeendelea kuwahimiza wananchi wote wakiwemo, wakulima, wafugaji na wavuvi kutumia fursa za uwepo wa umeme wa kutosha na wa uhakika ili kujiletea maendeleo.

Hayo yamesemwa leo na Meneja wa TANESCO Mkoa wa Simiyu, Injinia Khadija Abdallahmed kwenye banda la TANESCO katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Nyakabindi nje kidogo ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu.

Mhandisi Mradi wa Umeme wa Maji Julius Nyerere (JNHPP-2115) injinia Mwanji Mhaka,akitoa maelezo kwa wananchi waliofika kwenye banda la TANESCO kwenye maonesho ya Nanenane kwenye viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi mkoani Simiyu leo.Mpigapicha Wetu

“Naomba kutoa wito kwa Watanzania wote kwa ujumla wachangamkie hizi fursa za umeme na maendeleo ya kilimo, mifugo na uvuvi Tanzania nzima, umeme upo wa kutosha Tanzania nzima, TANESCO tupo tunaaangaza maisha,” Alisisitiza injinia Khadija.

Alisema TANESCO inashiriki maonyesho haya kwa vile wao ni wadau wakubwa wa shughuli za kilimo, mifugo pamoja na uvuvi na kwa huduma ya umeme itolewayo na shirika hilo ni sehemu ya kufanikisha maonesho hayo.

Aliwakaribisha wananchi wote wanaopata fursa ya kufika kwenye viwanja vya Nyakabindi yanakofanyika maonesho hayo kutembeela katika banda la TANESCO kwani watafaidika na kupata elimu kuhusu matumizi bora na sahihi ya umeme.

“Lakini wananchi watakaofika kwenye banda letu watakutana na mtaalamu mbobezi ambaye atawaeleza kuhusu mradi mkubwa wa kimkakati wa ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme Julius Nyerere (JNHPP 2115) kwenye bonde la mto Rufiji,” alisema.