April 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CWT kukipiga tafu chama cha walimu wanafunzi

Na Joyce Kasiki,timesmajira online,Dodoma

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Walimu Nchini (CWT) Mwalimu Deus Seif amesema chama hicho kipo tayari kusaidia mambo mbalimbali katika chama cha wanafunzi walimu cha Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOSTA) ili kiweze kujiendesha vyema na kufikia malengo yao.

Mwalimu Seif ametoa kauli hiyo wakati akifungua kongamano la walimu tarajali na kuwaaga wanafunzi walimu mwaka wa tatu lililofanyika katika kitivo cha Walimu katika chuo Kikuu cha Dodoma.

Akitoa majibu ya UDOSTA katika risala yao iliyosomwa na Katibu wake Emmanuel Pascal ,Mwalimu Seif amesema CWT kikiwa kama mlezi wa UDOSTA itawapatia photocopy mashine kwa ajili ya shughuli mbalimbali zinazohitaji huduma hiyo.
Licha ya kununua mashine hiyo pia amesema CWT kitachangia gharama za uendeshaji kila mwezi kupitia akaunti ya benki ya UDOSTA.

Vilevile Katibu Mkuu huyo amesema tayari Chama cha walimu kimeanzisha kitengo cha usimamizi na vyuo ili kiweze kuratibu shughuli za maeneo hayo vizuri.

Awali Katibu wa UDOSTA Emmanuel Pascal amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwake mwaka 2017 chama hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa vyanzo vya mapato na hivyo kufanya chama kujiendesha kwa michango ya wadau kikiwemo CWT.

Ameitaja changamoto nyingine kuwa ni wanachama (walimu) wanaojiendeleza wamekuwa wakikosa haki zao kama watumishi hasa katika suala la kuzuiwa kupanda madaraja .

Aidha Emmanuel amesema chama hicho hakina vifaa vya kisasa vya kutunzia kumbukumbu za wanachama jambo linalosababisha kupotea kwa taarifa za wanachama.

Katika risala yake,Katibu huyo ameomba CWT kiitambue UDOSTA kama mshirika wake ili kuwe na mkakati maalum wa kupewa semina mbalimbali za kukifahamu CWT na kujua haki za walimu lakini pia ifanyike utaratibu wa vyama vya walimuwanafunzi kusambaa katika vyuo vingine nchini kwani kwa sasa chama kama hicho kipo UDOM pekee.