May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANAPA yashauri wananchi kufanya utalii wa ndani

Na Joyce Kasiki, TimesMajira,Online Dodoma

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Nchini (TANAPA),limewaasa wananchi kujenga desturi ya kutembelea hifadhi mbalimbali zilizopo nchini ili kukuza uchumi wa nchi badala ya kusubiri wageni kutoka nje ya nchi kuja kufanya utalii hapa nchini.

Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi wa TANAPA Dodoma, Ahmed Mbugi ameyasema hayo wakati akifungua semina kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Dodoma iliyoandaliwa na shirika hilo ili kuwajengea uwezo wa kuandika habari zinazohusu utalii wa ndani katika hifadhi nchini ili nao waweze kuwaelimisha wananchi kuhusu utalii huo badala ya kusubiri wageni kutoka nje.

Kamishina Mbugi amebainisha kuwa wananchi wengi wamekuwa hawana uelewa wa kutosha kuhusiana na masuala ya utalii na hivyo wengi wao kudhani utalii unafwanywa na watu kutoka nje ya nchi pekee, huku wengine wakihofia gharama za utalii.

“Sisi wenyewe wananchi tunatakiwa kuwa wa kwanza kufanya utalii wa ndani kwa kutembelea hifadhi zetu hapa nchini,tusisubiri wageni, lazima na sisi tuchukue nafasi yetu kufanya utalii wa ndani ambao kwa kiasi kikubwa utachangia katika uchumi wetu,”amesema Kamishna Mbugi

Aidha ameeleza kuwa hifadhi zote nchini zina umuhimu na pia zina tofautiana pamoja na upekee wa aina yake na hivyo bado zina faida katika sekta nyingine.

Kwa upande wake, Kamishna Uhifadhi Msaidizi Mwandamizi wa Mawasiliano wa TANAPA, Paschal Shelutete ameelezea mafanikio ya hifadhi hizo toka kuanzishwa kwake Mwaka 1959 ikiwemo Kupungua matukio ya ujangili ya kuua wanyama.

“Haya ni mafanikio makubwa sana,zamani kulikuwa na matukio mengi ya kuuawa kwa wanyama hususan tembo,lakini sasa matukio hayo hayasikiki tena ,hii ni kutokana na kuimarishwa kwa ulinzi katika hifadhi zetu hapa nchini,”alisema Shelutete na kuongeza;

“Na kwa kipindi cha miaka miwili 2019 hadi 2020 hakuna tukio la kuuawa kwa tembo lililothibitishwa ndani ya mipaka ya hifadhi za Taifa .”

Amesema Shirika hilo linaendelea kuboresha mbinu za ulinzi ili kudhibiti ujangili wa tembo na wanyama wengine ndani na pembezoni mwa hifadhi za Taifa.

Aidha Shelutete amesema,ulinzi wa rasilimali za Taifa katika hifadhi na mapambano dhidi ya ujangili yanafanywa kwa mbinu za kisasa na weledi ikiwani pamoja na kufanya doria zinazoongozwa na taarifa za kiintelejensia na kutumia vifaa vya kisasa vya kielektroniki ambayo vimerahisisha kazi hiyo.

Naye Afisa Uhifadhi Mkuu wa Hifadhi za Taifa(TANAPA)Jully Lyimo amesema utalii husaidia kukuza uchumi na kipato kwa Taifa, kutambulisha nchi pamoja na kuongeza ajira.