May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tamisemi yaipongeza TET

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

TAMISEMI yaipongeza Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kuweka maudhui ya ujifunzaji na ufundishaji katika mifumo ya Kieletroniki

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais- TAMISEMI- Elimu, Dkt.Charles Msonde ameipongeza TET kwa kuweka maudhui ya Elimu ya Awali, Msingi , Sekondari na Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini katika mifumo wa kieletroniki, pamoja na kuweka vitabu vyote vya kiada katika Maktaba Mtandao.

Naibu Katibu Mkuu huyo ametoa pongezi hizo katika ziara yake ya siku moja aliyoifanya leo tarehe Desemba 18, 2022 katika ofisi za TET zilizopo jijini Dar es salaam.

Aidha, ameeleza kuwa ameguswa na kufurahishwa sana kwa TET kuweka vitabu vyote katika mfumo wa e-book jambo ambalo limerahisisha upatikanaji wa machapisho hayo na hivyo kurahisisha tendo la ufundishaji na ujifunzaji.

“Kwa kweli niwapongeze sana TET, hii ni hatua kubwa sana katika kuhakikisha upatikanaji wa vitabu kwa njia zote ikiwemo hii ya kupitia mifumo ya kieletroniki kilichobaki kwetu TAMISEMI ni kuhakikisha uwepo wa vifaa vya TEHAMA vitakavyowezesha wanafunzi wote nchini kuingia katika mifumo hii na kujifunza”amesema Dkt.Msonde.

Katika ziara hiyo Dkt. Msonde amepitishwa kwenye mifumo ya ufundishaji na ujifunzaji kwa walimu na wanafunzi pamoja na mfumo wa Maktaba Mtandao ya TET.

Pia alipata nafasi ya kutembelea studio za redio na television za TET pamoja na ghala la vitabu vya kiada lililopo EPZA ambako alielezwa namna kazi ya usambazaji na usafirishaji wa vitabu inavyofanyika.

Akiwa katika eneo la Maghala, Naibu Katibu Mkuu huyo ameipongeza TET kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuahidi kuhakikisha kuwa halmashauri zote nchini zinatoa takwimu sahihi za mahitaji halisi ya vitabu.

Katika hatua nyingine, Dkt. Msonde ameahidi ushirikiano kwa TET katika masuala yote hususani kwenye suala la mafunzo kazini kwa walimu na kwenye matumizi ya Maktaba Mtandao ambapo atawahamasisha viongozi na walimu katika Halmashauri zote kushiriki katika mafunzo na kutumia Maktaba Mtandao hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TET-Dkt. Aneth Komba amemshukuru Naibu Katiku Mkuu huyo kwa kutenga muda wa kuitembelea TET na kusema kuwa wataendelea kutekeleza kwa vitendo juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita.