May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Takukuru,Mwanza yabaini madudu asilimia 21 ya miradi ya maendeleo

Na Daud Magesa, TimesMajira Online, Mwanza

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)Mkoa wa Mwanza imefuatilia na kukagua miradi 130 ya maendeleo katika sekta mbalimbali yenye thamani ya bilioni 30.44 na kubaini asilimia 21 ya miradi hiyo ina kasoro.

Pia inachunguza taarifa 80 za malalamiko ya vitendo vya rushwa kati ya taarifa 137 zilizopokelewa kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2022 ambapo majalada 54 ya vitendo vya rushwa yamefunguliwa kati ya 80 yaliyokuwa yakichunguzwa.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza,James Ruge,amebainisha hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na utendaji wa taasisi hiyo katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2022,ambapo taarifa za vitendo vya rushwa zilizopokelewa zinaendelea kufanyiwa kazi na kuchunguzwa kwa mujibu wa sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa.

Wandishi wa habari wa vyombo mbalimbali leo wakifanya mahojiano an Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza, James Ruge (kushoto) kuhusu ufuatiliaji na ukaguzi wa miradi ya maendeleo mkoani humo.

Amesema wanachunguza miradi yenye kasoro ili wahusikawafikishwe mahakamani na wanachunguza taarifa 80 za vitendo vya rushwa zilizofunguliwa,majalada 54 yanakamilishwa na 26 uchunguzi wa awali unaendelea na kuwasihi wananchi kufuatilia elimu ya makosa ya rushwa na kupeleka tu malalamiko ya vitendo hivyo kwa mujibu wa sheria.

Aidha Ruge amesema upande wa mashitaka majalada matatu yamepata kibali cha Ofisi ya Mashitaka,kesi mpya mbili zimesajiliwa mahakamani na kufanya idadi ya mashauri 20 yanayoendelea mahakamani ambapo kesi sita ziliamuliwa na Jamhuri ilishinda nne na kushindwa mbili.

Pia amesema kwa kipindi cha Oktoba hadi Disemba wamefuatilia miradi ya maendeleo 130 katika sekta za elimu,afya,maji na ujenzi yenye thamani ya ya zaidi ya bilioni 30(30,437,923,228.13) kati ya hiyo,miradi 22 ya zaidi ya bilioni 6.5 (6,538,933,062.49) sawa na asilimia 21 ilibainika kuwa na kasoro,wahusika walishauriwa kuyarekebisha.

“Serikali imetoa mabilioni ya fedha kwenye miradi ya maendeleo lengo ilete ustawi kwa wananchi,kwa pamoja wananchi kwa ujumla wetu tunapaswa kufuatilia fedha za miradi hiyo kwa karibu ili lengo la serikali litimie,”amesema Ruge.

Amesema ujenzi wa vyumba 92 vya madarasa ya shule 12 za sekondari jijini Mwanza yanayojengwa kwa mfumo wa ghorofa kwa bilioni 2.5 walibaini kasi ni ndogo,ili yakamilike wamemshauri Mkurugenzi wa Jiji hilo atoe fedha kulinganana makadirio.

Pia kamati za ujenzi zizingatie sheria za manunuzi,wahandisi na kamati wayakamilishe madarasa hayo kwa wakati.

Pia wamemshauri Mhandisi wa Manispaa ya Ilemela kumwelekeza Mkandarasi wa Zahanati ya Mihama inayojengwa kwa thamani ya milioni 92.78 azingatiye maelekezo ya kitaalamu na BOQ baada ya kubaini msingi wake ni mfupi na eneo inakojengwa kuna chemichemi.

Mkuu huyo wa Takukuru amesema vyumba 11 vya madarasa vya sekondari ya Nyamadoke,Halmashauri ya Buchosa vinavyojengwa kwa thamani ya milioni 220,viwili vipimo vya urefu na upana havikuzingatiwa na kushauri fundi kuzingatia vipimo vya ramani na kurekebisha kasoro hizo,pia wamebaini mradi mkubwa wa Maji Sagani wilayani Magu wa gharama ya bilioni 2.506 mitaro ya kulaza mabomba imechimbwa kwa urefu usiotakiwa.

Mingine ni miradi minne ya milioni 389.9 ya matengenezo ya barabara zinazounganisha vijiji tisa vya Mantare-Mwanekeyi milioni37.46,Maligisu-Mwabasabi milioni 70.6,Manawa-Nyamigamba milioni24.2,Mhulula-Chamva-Mwabomba milioni 254.64 mkandarasi alitumia kifusi kisichostahili na kutakiwa kukiondoa.

Kwa mujibu wa Ruge kituo cha Afya Mwawile wilayani Misungwi kilichojengwa kwa gharama ya milioni 500,mkandarasi alikiuka utaratibu wa zabuni na kutumia saruji ya chini ya kiwango 32.5R badala ya 42.5N alicholipwa.

Uchunguzi unaendelea ukiwemo ujenzi wa matundu 24 ya vyoo shule ya msingi Mawemabi kwa gharama ya sh.milioni 40,zilitumika nondo za mm6 badala ya mm 8 na kutakiwa ziondolewe.

“Miradi iliyokaguliwa inatekelezwa vizuri,hivyo tunawaasa wakandarasi,wananchi na wote wenye dhamana wasimamie kwa ubora utekelezaji wa miradi mkoani Mwanza,watimize wajibu wao ipasavyo ili kutimiza adhima ya serikali kuhakikisha thamani ya fedha inazingatiwa ya kufikisha maisha bora kwa wananchi wake,”amesema.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza,James Ruge,leo akitoa taarifa ya utendaji wa taasisi hiyo kwa kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2022 kwa waandishi wa habari (hawapo pichani)