March 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Afya zapewa miezi mitatu kuhakikisha zina mikataba ya huduma kwa wateja

Na Mwandishi wetu,timesmajira,Online

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi ametoa muda wa miezi mitatu kwa Taasisi pamoja na Hospitali zote za mikoa, Kanda, na Taifa zilizopo chini ya Wizara ya Afya kuhakikisha zinakuwa na Mikataba ya Huduma kwa Wateja.

Prof.Makubi ametoa agizo hilo leo wakati wa uzinduzi wa Mkataba wa Huduma kwa wateja wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania uliofanyika katika Ofisi za Taasisi hiyo jijini Dar es salaam.

Katibu Mkuu Prof. Makubi amesema kuna baadhi ya Taasisi zimekaa muda mrefu bila kuwa na Mkataba wa Huduma kwa wateja licha ya utekelezaji wa mpango huo kuanza toka mwaka 2001 ambapo Taasisi zilitakiwa kutumia mikataba hii kwa utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi na tija zaidi.

“Wateja wetu wanaenda Hospitali na hawajui vipimo watapatiwa lini, unaenda maabara haujui majibu utayapata lini, matokeo yake inamlazimu mgonjwa kutumia njia zisizo rasmi”. alisema Prof. Makubi

Aidha Prof.Makubi amesema Mkataba huo una manufaa kwa Taasisi za Umma kwa ujumla ikiwemo wananchi kupata huduma kwa wakati na bila upendeleo kwani Taasisi zitalazimika kufuata viwango vilivyowekwa kwenye mkataba huo.

Awali akitoa neno la Ukaribisho Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna amesema Mkataba huo utawawezesha wateja wa Taasisi hiyo kuzifahahmu huduma zinazotolewa na Taasisi na utaiwezesha Taasisi kuboresha huduma zake kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu na pia kupata maoni au malalamiko kutoka kwa wateja na kuyashughulikia kwa wakati.

“lengo la Mkataba huu ni kuweka makubaliano kati ya Taasisi na wateja wetu juu ya wigo na viwango vya ubora wa huduma zinazotolewa ili kukidhi matarajio yao”amesema Dkt. Germana

Kwa upande wake Mwenyekiti Bodi ya usimamizi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Obey Assery amesema ameipongeza menejimenti ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa kuhakikisha wameandaa mkataba wa huduma kwa wateja kwani utasaidia kurahisisha utoaji wa huduma bora kwa kufuata viwango na hivyo kuwezesha Taasisi kutekeleza matakwa ya Serikali katika kuwahudumia wananchi.

Akitoa salamu kutoka kwa wadau wa lishe nchini Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali PANITA Tumaini Mikindo amesema hatua iliyochukuliwa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania ni muhimu kwani inamuwezesha mteja kufahamu ni huduma gani atazipata kwenye Taasisi hiyo na huduma gani hatozipata hivyo kumuondolea usumbufu wa kutafuta huduma hizo.

Mwaka 2001 Serikali ilianzisha utaratibu wa kutumia mikataba ya utoaji huduma kwa wateja ili kusaidia katika utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi na tija zaidi na mwaka 2013 serikali kupitia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ilitoa mwongozo katika utekelezaji wa mikataba ya utoaji wa huduma kwa wateja katika Taasisi za umma.