May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sukari yauzwa kama bangi Dar, mikoani

Wauzaji kuogopa kukamatwa, kilo sh. 4,000 maduka yaishiwa

Na Waandishi Wetu, Dar, Mikoani

WAFANYABIASHARA jijini Dar es Salaam na mikoani wameendelea kupuuza bei elekezi ya sukari iliyotangazwa na Serikali hivi karibuni, badala yake wameanza kuuza bidhaa hiyo kwa kificho na kwa watu wanaowafahamu ili kukwepa mkono wa sheria.

Wakati wafanyabiashara wengine wakiuza sukari kwa kificho na usiri mkubwa, bidhaa hiyo imeadimika kwenye maduka mengi rejareja, ambapo kwa walionayo wanauza kilo moja hadi sh. 4,000 jijini Dar es Salaam badala ya sh. 2,600 ambayo ndiyo bei elekezi.

Serikali ililazimika kutoa bei elekezi kufuatia wafanyabiashara wasio waaminifu kuficha sukari na kupandisha bei ya bidhaa hiyo kiholela na hivyo kuwaumiza wananchi.

Akizungumza jijini Dodoma hivi karibuni wakati akitangaza bei hiyo elekezi, Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga, alisema bei hizo zilipangwa kutokana na umbali wa mkoa ambapo kwa mikoa ya mbali hususani Kigoma na Katavi bei ya reja reja itakuwa 3,200, huku kwa Dar es Salaam bei iliyoelekezwa ni 2,600.

Waziri Hasunga alitoa onyo kali kwa mtu yoyote atakayeuza sukari kinyume cha bei elekezi. Pamoja na uamuzi wa Serikali kupanga bei elekezi kuleta faraja, hali ilivyo sasa ni kinyume na matarajio ya wananchi wengi ambapo wengine wamefananishwa stahili ya uuzaji sukari kwa sasa na ya uuzaji wa bangi.

Wauzaji wa bengi uwauzia watu wanaowafahamu kwa lengo la kujihami wasikamatwe na vyombo vya dola. Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi jijini Dar es Salaam wameutaka uongozi wa mkoa kuingilia kati bei ya sukari, vingine hali itazidi kuwa mbaya.

“Ninyi waandishi wa habari ndiyo watu wa kutusaidia. Kwa sasa sukari inauzwa kama bangi, kama wenye duka hawakufahamu hauziwi sukari,” alisema Anna Swai.

Alisema kwa sasa bei ya sukari imefikia sh. 4,000 na kibaya zaidi sio rahisi kuipata. “Dar tuliambiwa tutauziwa sukari kwa 2,600, lakini kwa sasa inauzwa hadi 4,000 tunaomba mamlaka za juu kuingilia kati jambo hili,” alisema.

Baadhi ya wauzaji wa reja reja waliozungumza na gazeti hili kwa sharti la majina yao kutochapishwa gazetini walisema kwa wauzaji wa jumla wanadai hawana sukari wakati wanawauzia watu wanaowafahamu kwa bei juu.

“Kwa hiyo ukibahatika kupata sukari hauwezi kuiuza kwa bei elekezi vinginevyo utapata hasara,” alisema mmoja wa wafanyabiashara hao. Waandishi wetu katika mikoa mbalimbali wamethibitisha kwamba licha ya bidhaa hiyo kuandimika, bei elekezi iliyotangazwa na Serikali nayo haizingatiwi.

Mkoani Morogoro, Mkuu wa Mkoa huo, Loata Ole Sanare akizungumza mwishoni mwa wiki alisema hakuna sababu ya msingi inayopelekea sukari kukosekana mkoani humo. Aliwalaumu baadhi ya wafanyabiashara wa maduka makubwa kwa kuuza sukari kwa kuficha kwenye maghala yao.

Sanare alitoa kauli hiyo alipokutana na wafanyabiashara wanaouza sukari kwa bei ya jumla kwa lengo la kujadiliana sababu za kukosekana kwa sukari madukani ndani ya mkoa huo.

Alisema kuna baadhi ya wafanyabiashara wanauza sukari kwa bei ya juu ili kupata faida zaidi jambo ambalo mfanyabiashara wa rejareja akinunua kwao hataweza kuuza kwa bei elekezi iliyotolewa na Serikali, hivyo aliwataka wafanyabiashara hao kufuata utaratibu.

Loata aliwataka wafanyabiashara walioficha sukari kwenye maghala kuitoa na kuiuza kwa bei halali kulingana na bei elekezi na kufuata taratibu zote za Serikali ikiwa ni pamoja na kutoa risiti kwa mnunuaji ili wasisingiziwe chochote na wafanyabiashara wadogo kwa kuwa risiti itawalinda.

“Hakuna sababu ya sukari hapa Morogoro kuuzwa juu ya bei elekezi, hakuna hata kidogo, lakini kwa taarifa nilizo nazo na nyaraka nilizonazo hapa hakuna sababu yoyote ile ya sukari kutokuwepo madukani,”alisema Sanare.

Aidha, aliwataka wafanyabiashara hao wenye maduka makubwa kukaa pamoja na kukubaliana bei moja itakayotumika kuuza sukari yao, bei ambayo haitawabana wafanyabiashara wadogo, badala yake iwawezesha kuuza kwa bei elekezi inayowapa faida na wao.

Pia aliwataka maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Morogoro kusimamia zoezi la upatikanaji wa sukari, na kwamba hatapenda kusikia tena kero ya sukari katika mkoa wake badala yake watumie sheria walizonazo kubaini sukari iliyofichwa katika maghala na kuchukua hatua dhidi ya walioificha.

Nao wafanyabiashara wakizungumza kwenye kikao hicho walisema kukosekana kwa sukari kunatokana na mkanganyiko wa bei elekezi.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Hussein Binzoo alisema kukosekana kwa sukari kulisababishwa na mkanganyiko wa bei elekezi iliyotolewa na Bodi ya Sukari iliyoelekeza
bei ya mfuko mmoja wa kilo 50 mkoani Morogoro uuzwe kwa sh. 127,500 wakati wao wananunua Dar es Salaam kwa sh. 127,000 jambo ambalo walisema bei hiyo ni hasara kwao.

Binzoo aliwaomba maofisa wa Serikali mkoani humo kuwa na mahusiano ya karibu na wao kwa kuwa wao ni wadau wa Serikali na wasiwaone kama maadui wa Serikali jambo ambalo liko miongoni mwa maofisa hao.

Naye mfanyabiashara aliyejulikana kwa jina moja la Mloso, alisema majira ya masika yakikaribia kila mwaka viwanda vya sukari vingi husimamisha uzalishaji wake, hivyo aliiomba Serikali wakati wa kipindi hicho Serikali iwaruhusu wafanyabiashara wanaosambaza sukari kuagiza sukari nchi za nje kwa wingi ili kuondoa adha ambayo hutokea kila mwaka.

Aidha, wafanyabiashara hao waliiomba Serikali kudhibiti mgawanyo wa sukari kutoka viwandani na kwa wafanyabiashara wakubwa, kwani wakati mwingine pamoja na mgawanyo wa sukari kutolewa huwa haifiki kwa walengwa au eneo husika.

Ofisa Biashara Mkoa wa Morogoro, Gerhard Haule, alisema atafuatilia kwa karibu mgao wa sukari unaotarajiwa kuja kwa siku za karibuni na kwamba atahakikisha kila mfanyabiashara anapata sukari hiyo, ili kuondoa kero iliyowasilishwa na wafanyabiashara hao.