April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Stakabadhi ghala yavunja minyororo ya madalali,yawainua Wakulima

Na Mwandishi wetu ,Timesmajira

Mfumo wa stakabadhi za ghala umeendelea kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo nchini, kwa kuboresha upatikanaji wa masoko ya mazao na kuongeza kipato kwa wakulima.

Kupitia mfumo huo, wakulima wameondokana na changamoto ya kulanguliwa mazao yao na madalali, hali iliyokuwa ikiwanyima faida halisi ya jasho lao. Sasa, mazao yanauzwa kwa uwazi kupitia bei za soko, jambo linalowawezesha wakulima kupata tija stahiki.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Asangye Bangu, amesema mfumo huo umeimarika kwa kiasi kikubwa na sasa unatekelezwa katika mikoa 23 kati ya 26 ya Tanzania Bara, ukihusisha bidhaa 18 tofauti.

Amesema mafanikio ya mfumo huo yanaonekana wazi kwa wakulima pamoja na Halmashauri kupitia ongezeko la ukusanyaji wa mapato.

“Kwa sasa mfumo umeboreshwa, unafanya kazi kwa ufanisi na tija inaonekana kwa wazalishaji na serikali za mitaa,” amesema Bangu.

Ameeleza kuwa ukusanyaji wa mazao unafanywa kupitia vyama vya ushirika pamoja na wafanyabiashara wenye leseni, ambao hapo awali walitambulika kama madalali. Tofauti na zamani, wanunuzi hao sasa hununua mazao kwa bei ya ushindani na uwazi zaidi.

Aidha, mazao yote yanayoingizwa kwenye maghala huwekwa katika kanzidata ya bodi hiyo, ambayo hutumika pia na Soko la Bidhaa Tanzania katika kuuza mazao kidijitali. Ushirikiano huo umeongeza ufanisi na kuleta manufaa makubwa kwa wadau wote wa sekta hiyo.

“Kwa umoja wetu tunaweza kuhakikisha mkulima anapata soko lenye tija na kurejea na faida ya jasho lake,” amesisitiza Bangu.

Kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya tani 400,000 za korosho zimeuzwa kupitia mfumo huo, huku mbaazi zikifikia zaidi ya tani 200,000, ufuta tani 200,000 na choroko zaidi ya tani 60,000.

Bangu amesema hata mazao ambayo awali hayakuchukuliwa kama ya biashara, sasa yamekuwa chanzo muhimu cha kipato kwa wakulima na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Mbali na hilo, mfumo huo umeongeza ushirikishwaji wa wakulima katika sekta ya fedha kwa kuwawezesha kutambulika na taasisi za kifedha, hivyo kupata mikopo kwa urahisi zaidi.

“Kimsingi tumerasimisha biashara ya mazao na kuwapa wakulima hadhi rasmi kiuchumi,” amesema.

Pia, mfumo huo umechangia ajira kwa vijana, ambapo kila ghala linakadiriwa kuwa na angalau wafanyakazi watano, wengi wao wakiwa wahitimu wa vyuo vikuu.

Bodi hiyo inaendelea kuwekeza katika ujenzi na uboreshaji wa maghala pamoja na kusajili maghala mapya ili kuongeza ufanisi wa soko la ndani.

Kwa upande wa udhibiti wa ubora, Bangu amesema jukumu hilo linatekelezwa na wasimamizi wa maghala, wanaohakikisha kuwa mazao yote yanayohifadhiwa yanakidhi viwango vinavyotakiwa kabla ya kuuzwa.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa wakulima hawalazimishwi kutumia mfumo huo isipokuwa kwa mazao yenye bodi maalum za usimamizi, ambapo ni lazima kufuata utaratibu uliowekwa.

Ametoa wito kwa wadau wa kilimo kushiriki maadhimisho ya miaka 20 ya mfumo huo yatakayofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma kuanzia Aprili 28 hadi 30 mwaka huu.

Akizungumzia historia ya mfumo huo, Bangu amesema ulianza kufanyiwa utafiti tangu mwaka 2000 kabla ya kuanzishwa rasmi kupitia sheria mwaka 2005 na kuanza kutekelezwa mwaka 2006.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi wa WRRB, David Sukali, amesema mfumo huo umeongeza upatikanaji wa mikopo kwa wakulima na kuboresha ushindani wa bei sokoni.

Amesema pia mfumo huo umeongeza ukaribu kati ya wakulima na soko, hivyo kurahisisha uuzaji wa mazao kwa haraka na kwa bei yenye tija.