Na Mwandishi Wetu, Arusha
MABINGWA mara tatu mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) timu ya Simba wamefanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii baada ya kupata ushindi wa goli 2-0 dhidi ya Namungo katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Hii ni mara ya sita na mara ya nne mfululizo Simba inatwaa Ngao hiyo na kuweka rekodi ya kuwa timu iliyotwaa taji hilo mara nyingi zaidi toka mwaka 2001 wakifuatiwa na Yanga waliotwaa Ngao hiyo mara tano.
Simba SC ilibeba Ngao hiyo mwaka ya 2011 ikiifunga Yanga 2-0, 2012 wakiwafunga Azam goli 3-2, mwaka 2017 wakiwafunga tena Yanga kwa penalti 5-4 baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu ya bila kufungana, mwaka 2018 waliwafunga Mtibwa Sugar goli 2-1 pamoja na mwaka 2019 ambapo waliwafunga tena Azam goli 4-2.
Katika mchezo huo Nahodha John Bocco ndiye aliyekuwa wa kwanza kuipatia timu hiyo goli la kwanza kwa mkwaju wa penalti dakika ya saba baada ya winga Mghana, Benard Morrison kuangushwa kwenye eneo la 18.
Goli hilo liliwaamsha Namungo ambao nao walianza kulishambulia kwa kasi lango la wapinzani wao Simba am bao nao walijibu mashambulizi ambayo yaliokolewa na kipa Nourdine Balora akisaidiana na mabeki wake.
Licha ya Simba kupambana kusaka goli la pili lakini Namungo ambao nao walionesha kiu ya kusawazisha walipambana lakini hadi kipindi kwa kwanza kinamalizika jitihada zao zilishindwa kuzaa matunda.
Kipindi cha pili Morrison aliifungia Simba goli la pili dakika ya 60 akimalizia pasi ya kiungo Mzambia, Clatous Chama.
Katika mchezo huo pia, kiungo Jonas Mkude alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mchezo huo na kuzawadiwa tuzo pamoja na kiasi cha Sh. 500,000.
More Stories
Watumishi wa Fahari wafanya Bonanza
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship