May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yanga waendelea kumng’ang’ania Morrison

Na Mwandishi Wetu

WAKATI winga Benard Morrison akiitumia klabu yake mpya ya Simba katika mchezo wa kwanza wa Ngao ya Jamii na kuonesha kiwango bora baada ya kupata kibali kipya cha kazi, Uongozi wa klabu ya Yanga umesema bado wanatambua kuwa mchezaji huyo ni mali yao na kumtambulisha katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Mwananchi yaliyofanyika katika Uwanja wa Mkapa.

Katika utambulisho wa wachezao wao wapya wa ndani, wa nje ya nchini pamoja na wale waliokuwepo msimu uliopita, Muongozaji wa shughuli hiyo, Maulid Kitenge ameweka wazi kuwa bado Yanga inatambua kuwa Morrison ni mchezaji wao.

Kitenge amesema, “Waswahili wana msemo wao wanasema Mke ambaye hujampa talaka bado ni mkeo hivyo mchezaji wa 28 ndani ya Yanga ni Bernard Morrison ambaye ni mchezaji wetu kwa kuwa kesi ipo CAS hivyo ni mchezaji wa Yanga.”

Kauli hiyo ya Kitenge iliibua shange kwa mashabiki wa klabu hiyo ambao jana walijitokeza kwa wingi na kuujaza uwanja huo wa tofauti na ilivyokuwa kwa wapinzani wao Simba.

Licha ya Yanga kumtambulisha Morrison kuwa bado ni mchezaji wao, Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ya Wiki ya Mwannchi ambaye pia ni Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ameutaka uongozi wa klabu hiyo kutopoteza muda na kesi hiyo.

Kikwete amesema kuwa, suala la kuibiana wachezaji lipo toka enzi na enzi na wala halijaanza kwa Morrison na hili la kupeleka FIFA ni kupoteza muda.

“Hili suala la kuibiana wachezaji lipo toka enzi na enzi na wala halijaanza kwa Morrison kama mmeibiwa na nyie tafuteni wa kuwaibia sio mnalalamika tu, mnapoteza kuda kushtaki mpata FIFA, ” amesema kiongozi huyo.

Katika hotuba yake pia, kiongozi huyo amesema kuwa, amefurahishwa na maandalizi pamoja na kutambua mchango mkubwa unaotolewa na wadhamini ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya Yanga na kuwasihi kuendelea kuiunga mkono.