January 19, 2022

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Siku ya kuzaliwa Nyerere na zawadi ya kurejesha NMC

BABA wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizaliwa April 13,1922, Watanzania wanapokumbuka kuzaliwa kwake Serikali ya Awamu ya Tano imehakikisha inamkumbuka kwa zawadi ya pekee ya kufufua Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC).

Waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Kilimo na Chakula Japhet Hasunga,Aprili 5, 2020, anasema “Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (Cereal and Produce Board (CPB) imerejesha Shirika la Usagishaji la Taifa (National Milling Cooperation (NMC).

Shirika ambalo liliweza kutoa huduma wakati wa kipindi kigumu cha ukame,njaa na mikiki ya migogoro ya uchumi duniani na kulifanya kuwa mkombozi mkubwa wa Watanzania kwa kutoa huduma,kipindi cha Awamu ya Kwanza ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere”.

Akiainisha msukumo wa kufufua Shirika hilo Waziri Hasunga anasema kuwa Serikali iliona ipo haja ya uhifadhi wa chakula kwenda sambamba na uwepo wa Shirika la Usagishaji la Taifa,ili kuwahudumia Watanzania kama ambavyo ilikuwa ikifanya kipindi cha Awamu ya Kwanza.

Aidha, akithibitisha kufufuliwa kwa Shirika hilo, Waziri Hasunga ameongeza kusema kuwa, hivi sasa Bodi ya Mazao Mchanganyiko imeamua kurejesha vinu na mali zote ambazo awali zilibinafsishwa na kukabidhiwa kwa watu binafsi, ambapo Bodi inasaga unga wa mahindi kwa ajili ya chakula ukiwemo unga halisi wa mahindi unayotokana na mahindi yenye ubora unaofaa kwa matumizi ya chakula cha binadamu.

“Unga huu umethibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa ajili ya matumizi ya binadamu ambapo sasa bodi hiyo inasaga unga bora wa dona ulioandaliwa pasipo kuondolewa maganda na hivyo kuufanya unga huo kuwa na protini ya kutosha na mafuta kwa ajili ya kuupa joto mwili wa mlaji”, anasema Hasunga.

Anaongeza kuwa dona bora husagwa kwa kutumia mashine maalum ili kupata unga safi na wenye kiini stahiki wenye virutubisho vyenye protini,wanga na vitamini vinavyozuia utapiamlo na unyafuzi kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Katika kuhakikisha NFRA inakuwa mkombozi wa kweli,Waziri Hasunga anasema kuwa Wakala unapaswa kubadili dhana ya kununua mahindi kwa ajili ya hifadhi pekee badala yake wanapaswa kununua mahindi kwa ajili ya kuyauza ili kuongeza ufanisi wa soko kwa wakulima nchini.

Katika hatua nyingine anasema kuwa tayari NFRA imeanza kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa kununua na kuuza mahindi kupitia mkataba na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) utakaopelekea wao kurejea sokoni kununua mahindi kwa wakulima na kuondoa adha ya soko kwa kushirikiana na CPB.

Siku za nyuma NFRA ilikabidhiwa mtambo wa kusafisha nafaka na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wenye thamani ya Dola za Marekani 170.841 sawa na Shilingi za Tanzania milioni 399.8.

Mtambo huo una uwezo wa kusafisha mahindi zaidi ya tani 100 kwa siku. Hii imetokana na WFP kuichagua Tanzania kuwa moja wapo ya Kituo cha Usimamizi wa Bidhaa za Kimataifa (Global Commodity Managed Facility) ambacho kinasaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa masoko ya mazao ya chakula kwa wakulima nchini.

“Mpango Mkakati wa WFP wa miaka mitano (Country Strategy Plan 2017-2021) unaendana na mipango ya Serikali inayolenga kufikia Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDGs),hususani lengo la kutokomeza njaa (zero hunger) ifikapo mwaka 2030” anasema.

Jambo hili la kurejesha na kufufua NMC kwa Baba wa Taifa Nyerere ni ushindi mkubwa sio tu kwa kuwa ni mwanzilishi na mbunifu wa shirika hilo,bali ni kutokana na umuhimu wa shirika hilo katika kulinda usalama wa chakula kwa nchi iliyo huru na kuweza kuwahudumia wananchi wake bila kuwa tegemezi pindi dharura inapotokea.

Utegemezi hususan nyakati za shida ni jambo linalohatarisha uhuru na udhibiti wa nchi,ipo mifano mingi sana hapa duniani inayoonyesha unapokuwa na shida mtu au nchi inaweza kukupa masharti magumu ili waweze kukupatia chakula. Wewe kama kiongozi unapoona wananchi wako wana shida ya njaa na ili uondokane na hiyo njaa huna budi kuyakubali masharti uliyopewa ili kunusuru raia wako.

Aidha,uwepo wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA),ulikuwa sahihi lakini maafa hayapigi hodi kuwa nakuja,mfano wananchi wamepata mafuriko vitu na nyumba zao zimekwenda na maji,unapompa mahindi wakati hana hata hakiba ya fedha, nyumba na mahali pa kujisitiri hawezi kukoroga hata uji akawapa watoto wake, mpaka atafute huduma ya kusaga mahindi aliyopewa hiyo inakuwa sio huduma ya kumsaidia anaye hitaji msaada kwa haraka.

Hivyo,suala la kufufua na kurejesha NMC, ni jambo la kupongezwa na Watanzania wote wanaoipenda nchi yao kwa kuwa NMC ni mkombozi na njia ya kuongeza suala la usalama wa Taifa letu , kwa kuwa mabeberu bado wapo na hawaitakii mema nchi yetu watakapopata mwanya wa kuona tunatetereka na kuomba msaada kwao hapo hapo watajipenyeza na kuingiza agenda zao.

Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliona mbali kuliko mimi na wewe tunavyofikiria, nina hakika Serikali ya Awamu ya Tano wameliona hili na kuliweka katika mzani na kuhakikisha hawaliachi Taifa letu kwenda mrama na kuzama kwa kuwa usalama wa Taifa letu ni muhimu sana kwa mstakabali wa vizazi wa sasa na vya baadaye.

Hakika Serikali ya Awamu ya Tano imempa zawadi ya kipekee Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na kuifanya siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake tarehe 13, April 2020 kuwa ya kipekee na inayompendeza kila Mtanzania, “Heri ya Kuzaliwa Mwalimu”, falsafa, mawazo yako, fikra zako, mtazamo wako, na utendaji wako utabaki kuwa dira na muongozo katika Taifa hili.

Awamu ya Kwanza ya uongozi imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha Taifa hili linakuwa salama na kuhakikisha wazalendo wanayoipenda kwa dhati nchi ya Tanzania wanaendelea kuwa viongozi wa nchi kwa masilahi mapana ya Watanzania wote. Baada ya kubinafsisha NMC Tanzania ilibaki na NFRA ambazo hifadhi hizo zipo katika Kanda Kuu za Uzalishaji wa Chakula ambapo mazao yanayonunuliwa ni pamoja na mahindi, mtama na mpunga.

Bodi ya CPB kwa sasa inasimamia Kanda saba ikiwemo Kanda ya Ziwa yenye mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Simiyu, Geita na Shinyanga, Kanda ya Mashariki mikoa ya Dar-es-salaam, Pwani, Tanga, na Morogoro, Kanda ya Kati mikoa ya Singida na Dodoma. Nyingine ni Kanda ya Kaskazini yenye mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, Kanda ya Kusini ni Mkoa wa Lindi na Mtwara, Kanda ya Magharibi ina mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi na Nyanda za Juu Kusini ni Mbeya Iringa Njombe Rukwa na Ruvuma.

Watanzania wanapokumbuka kuzaliwa kwako Mwalimu Nyerere, tunasukumwa na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt.John Magufuli ilioazimia kuzifuata nyayo zako na kutekeleza kwa vitendo kila ulichokiasisi na kukiasa hakika Heri ya kuzaliwa Mwalimu Nyerere na pokea zawadi ya kufufuliwa NMC.