December 7, 2021

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SHIWAKUTA latakiwa kuwaendeleza wakulima wafikie malengo yao

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma 

SERIKALI imelitaka Shirikisho la Vyama vya wakulima wadogo nchini (SHIWAKUTA) kufanya kazi yake kwa weledi na kuondoa malalamiko ya wananchama ili kusogeza mbele sekta ya kilimo,mifugo na uvuvi.

Hayo yamesemwa leo na Mkuugenzi Msaidizi ,uendelezaji wa Mazao ,pembeeo na Ushirika kutka wizara ya Kilimo Beatus Malema wakati akifungua mkutano Mkuu wa  kwanza na kuzindua Shirikisho hilo jijini Dodoma 

Amesema, kuungana kwao na hatua waliyoichukua yakuanzisha shirikisho hilo ni  sehemu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ya  kuhakikisha kuwa wazalishaji wadogo vijijini wanaungana kupitia vikundi, ushirika, mitandao, jumuiya,na mashirikisho kwa ajili kufanikisha vita ya kumpiga adui umaskini na kujiletea maendeleo.

“Kwa hiyo kuungana kwenu ni kuisiadia Serikali katika kuinua sekta ya kilimo,mifugo na uvuvi ,hivyo sitarajii wala sitegemei kupokea mlalamiko kutoka kwa mtu yeyote kuhusu kudhulumiwa haki yake.ämesema Malema

Aidha amesema,katika kuelekea maadhimisho ya  miaka 60 ya Uhuru, historia inatuonesha kuwa kundi la wakulima, wafugaji na wavuvi wadogo vijijini limeendelea kuwa nguzo ya umoja wa kitaifa sambamba na kuwa mhimili wa uhakika na usalama wa chakula.

“Wamekuwa wazalishaji waaminifu wa mazao ya chakula na biashara hali iliyopelekea taifa letu kujitosheleza kwa chakula huku pakiwa na ziada inayouzwa nje na hivyo kuchangia pato la taifa kwa zaidi ya asilimia 25.”amesema na kuongeza kuwa

“Takriban asilimia 65 ya malighafi zinazotumiwa na viwanda hapa nchini zinanatokana na mazao ambayo kwa kiasi kikubwa yanazalishwa na wakulima wadogo..,hivyo kwa  kuzingatia ukweli huo, sio rahisi kutenganisha utulivu na uimara wa kisiasa nchini kwa muda wote wa miaka 60 ya Uhuru na mchango mkubwa unaotolewa na wakulima, wafugaji na wavuvi wadogo vijijini.

Kwa mujibu wa Malema, Serikali inatambua na kuunga mkono vyama vya kijamii vikiwemo vya wakulima na ndio maana imeweka utaratibu wa kuvisajili na kuvisimamia ili vitekeleze shughuli zao kwa mujibu wa sheria za nchi.

Amesema siyo  tarajio la Serikali kuona vyama vya wakulima vikitumika kwa maslahi ya wachache badala ya wanachama walio wengi, au kujielekeza katika masuala ambayo siyo yaliyopelekea kusajiliwa kwake.

“Tegemeo la Serikali ni kuviona vyama vya wakulima vikiendeleza maslahi ya wanachama wake na kuwa wabia waaminifu katika kuchangia maendeleo ya taifa.”amsisitiza

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho hilo Marselina Charles amesema lengo kuu la kuundwa kwa shirikisho hilo ni kuwaunganisha pamoja wakulima, wafugaji na wavuvi wadogo vijijini kupitia jumuiya zao ili kujiletea maendeleo na kuwa na sauti ya pamoja katika kutetea maslahi yao.

“Dhamira hiyo ya kuwa pamoja ina lengo la kuendeleza na kulinda maslahi yetu kupitia jumuiya zetu ili kujiletea maendeleo na kuwa na sauti ya pamoja katika kutetea maslahi yetu.”Amesema Marselina

Awali Mratibu wa SHIWAKUTA Richard Masandika amesema, Shirikisho hilo ni  taasisi mpya nchini Tanzania ikiwa na lengo kubwa la kuvileta pamoja vyama vya wakulima vya Tanzania vilivyosajiliwa kama Jumuia za Kijamii zikiwa zinafanya kazi za uzalishaji katika kilimo, ufugaji na uvuvi kwa ujumla wake na pia zilizosajiliwa kufanya kazi za kuwezesha wazalishaji wadogo hapa nchini.

“Utafiti mdogo uliofanyika na baadhi ya waanzilishi wa SHIWAKUTA ulionyesha kuwepo kwa nakisi ‘gap’ kwenye eneo hili ambapo vyama vingi vilivyoandikishwa na kufanya kazi na wakulima, wafugaji na wavuvi wadogo havikuwa vimeunganishwa na chombo chochote ili kuleta muunganiko wa yale wanayoyafanya na hata kukosekana kwa sauti ya pamoja inapofikia haja ya kupaza sauti kwa ajili ya suala linalomtatiza mmoja au wote.”

Aidha amesema  SHIWAKUTA ilisajiliwa rasmi kama Jumuiya ya Kijamii  mnamo Juni  17 , 2021 ambapo  Makao Makuu ya muda ya  shirikisho hilo yapo mkoani Arusha .

Kwa mujibu wa Mratibu huyo,Shirikisho hilo limeundwa na vyama  12 ambavyo ni pamoja na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji Mkoa wa Kilimanjaro (MVIWAKI),Mtandao wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji Mkoa wa Arusha (MVIWAARUSHA), Kagera Women Environmental Society (KAWESO) ,Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Mkoa wa Kagera (MVIWATAKAGERA), Umoja wa Wakulima wa Umwagiliaji Ndanda (Mtwara) na Tanzania Grape Growers Association – TAGGA (Dodoma) .

Vyama vingine vilivyounda shirikishohilo ni Chama cha Wakulima wa Mpunga Tuungane (Tuungane Rice Farmers Association),Umoja wa wakulima wa Umwagiliaji Mkungu (Mtwara),Uhuru Coffee group (Songwe),Mshikamano Cofe group  (Songwe),Jumuia ya Wakulima na Wafugaji Wadogo Ruvuma (JUWAWARU) na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji wa Mkoa wa Manyara (MVIWAMA).