April 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shirika la Posta latakiwa kufanyia kazi changamoto za wafanyakazi wake

Na Rose Itono ,timesmajira,Online


NAIBU Waziri wa  Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew amelitaka Shirika la Posta Tanzania(TPC) kuzifanyia kazi chagamoto zinazowakumba Wafanyakazi wake hususani vitendea kazi kwani wao ndio chachu ya mafanikio.


Agizo hilo amelitoa Mkoani  Dar es Salaam wakati akifunga kikao kazi cha kutathimini utendaji kazi wa Viongozi wa Shirika la Posta Tanzania  ambapo amesema wafanyakazi wa ngazi za chini wengi wao wamekuwa wakikumbana na chagamoto ya vitendea kazi wawapo kazini na kupelekea kushidwa kutimiza majukumu yao vizuri.

“Watendaji wa ngazi ya chini  hususani wale wa mikoani wamekuwa  wakishindwa kufanya kazi zao vizuri kutokana  kukosa vitendea kazi ikiwemo gari na vifaa vya kidigitali kama simu kompyuta ili waendane na kasi ya ukuaji wa Teknolojia.


Mhandisi Mathew amesema ipo  haja ya uongozi wa juu wa Shirika la Posta Tanzania kuhakikisha kuwa unawapatia vifaa hivyo ili wawe katika mazingira rafiki ya utendaji kazi na kuendana na kauli mbinu ya Shirika ya “twenzetu kidigitali”.


Aidha amewataka wafanyakazi wa Shirika hilo kujitoa katika kuhakikisha kuwa Shirika linakuwa na kuiletea serikali faida huku akiwapongeza baadhi ya wafanyakazi wa Shirika hilo wanaofanya vizuri na kuwasisitiza kuendelea kushirikiana kwa pamoja ili kuwa na utendaji wenye ufanisi.


Katika hatua nyingine  ameliagiza Shirika la Posta Tanzania  kupitia sera na sheria mbalimbali ikiwemo ile ya shirika  la posta ili waweza kutengeneza mifumo bora ya TEHAMA  kwa ajili ya uendeshaji wa Shirika kwa bei nafuu na kuhakikisha inafanya kazi vizuri na kwa ufanisi.


Kwa upande wake Posta Master Mkuu Macrice Mboda amesema kuwa katika mkataba wa utendaji kati ya shirika na Katibu Mkuu wa ofisini ta Mawasiliano na Teknolojia ya Habari mambo yanayotakiwa kutekeleza na majukumu ya Shirika kwa mwaka 2021/ 2022 waliona ni vyema wakutane kwa pamoja na viongozi wa vyama vya wafanyakazi ili watafakari na kusainiana mikataba ya utendaji kwa mwaka 2021/22.


Aidha amesema lengo lao ni kuhakikisha kuwa Shirika la posta linafikia na kutekeleza maono ya serikali ya posta ya kidigitali ambapo malengo makuu 12 walioyafanya ikiwemo mafunzo ya kufanya kazi kwa ushirikiano, mafunzo ya serikali mtandao, kuheshimu itifaki, utunzaji wa siri za serikali pamoja na kuingia makubaliano ya kibiashara kati ya shirika na benki ya CRDB.


Amesema  kuwa ili kuhakikisha kuwa dira na mwelekeo wa serikali katika sekta hiyo yanafanikiwa wamesainiana mikataba ya utendaji na viongozi wa makao makuu na mikoa ili kufanikisha malengo ya mwaka 2021 na 2022.