May 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shabaha ya kipindi cha Konzi la Moyo TV Show,kutatua suala la ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi miaka 6-21

Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Imeelezwa kuwa miongoni mwa makundi yanayokumbana na vitendo vya ukatili ni pamoja na wanafunzi wenye umri wa miaka 6 hadi 21.

Hivyo katika kuhakikisha changamoto hiyo ya ukatili kwa kundi hilo inatatuliwa Mwandishi Nguri wa Habari Florah Magabe akishirikiana na Mwalimu wa Waandishi wa Habari Dotto Bulendu,wameandaa kipindi cha Konzi la Moyo TV Show cha dakika 10 ambacho kitasambazwa katika mitandao ya kijamii.

Akizungumza jijini Mwanza wakati wa uzinduzi wa kipindi hicho ambacho kilizinduliwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Sam Rumanyika,Muuandaaji wa kipindi hicho Florah Magabe amesema,shabaha ya kipindi hicho ni kutatua suala la ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi wenye umri wa miaka 6 hadi 21 katika Mkoa wa Mwanza.

Florah amesema, kipindi hicho kitatoa uwanja wa kuibua matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa wanafunzi wa rika la miaka 6 hadi 21 kupitia uandaaji wa vipindi 366 na kuvisambaza katika mitandao ya kijamii kuwafikia wadau 256,000 kupitia vikundi 1,000 songozi vya mtandao wa kijamii wa WhatsApp.

Amesema,kipindi hicho chenye dira ya kutengeneza jamii inayoheshimu utu na haki za binadamu kitakachokuwa kinaruka kila siku kwa muda wa mwaka mzima kupitia mitandao ya kijamii .

“Utafiti uliofanywa na Muasisi wa kipindi hiki katika shule 100 na vyuo 21 katika Mkoa wa Mwanza na Simiyu ni kubaini kati ya wanafunzi 10,6 kati yao wamekutana na ukatili wa kijinsia ikiwemo wa kujamiana pamoja na kujeruhiwa mwili,” amesema Florah.

Akizindua kipindi hicho Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Sam Rumanyika, amesema sheria ya mtoto inasema mtoto ni mtu yoyote mwenyewe umri chini ya miaka 18,hivyo Halmashauri zitunge Sheria ndogo ndogo ambazo zitawabana wazazi au walezi ambao wanatabia ya kuozesha watoto katika umri mdogo.

Rumanyika,amesema wanahabari washike kalamu zao kwa ajili ya kusaidia jamii hili iondokane na vitendo vya ukatili.

Kamishina Msaidizi wa Polisi ambaye ni Ofisa Ushirikishwaji Jamii Polisi Mkoa wa Mwanza Hamisi Mwampelwa, alieleza kuwa ukatili wa kijinsia hauchagui chama wala dini hivyo jamii isinyamaze inapoona ama kusikia taarifa za ukatili wa kijinsia .

“Tukishirikiana wote kwa pamoja, unyanyasaji,ukatili wa kijinsia na udhalilishaji wa watoto janga hili litakwisha, tukishirikiana sote ngazi ya Jamii,Kijiji,mtaa,kata, Halmashauri,Wilaya hadi Mkoa,” amesema Mwampelwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika la Haki Zetu Tanzania Gervas Evodius, amesema,sehemu ambayo kuna upendo kuna amani hakuna ukatili hivyo wataendelea kushirikiana na muandaaji wa kipindi hicho ili kupinga ukatili na kuhakisha Kuna kuwa na jamii salama.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilangi,alieleza kuwa ndani ya jamii kuna mambo mengi likiwemo la ukatili hivyo watahakikisha wanapambana na jambo hilo.

“Serikali itatoa ushirikiano wa hali ya juu katika kukiendeleza kipindi chako cha konzi la moyo kwa sababu kitasaidia jamii kuondokana na vitendo vya ukatili,” amesema Makilagi.

Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Stanslaus Mabula amesema ubunifu wa kipindi hicho ni muhimu katika jamii na litakuwa ni daraja la kujifunza hivyo watashirikiana kuhakikisha jamii inapona na janga hilo.

Mwandishi Nguri wa habari, Muandaaji wa kipindi cha Konzi la Moyo TV Show Florah Magabe kulia akiwa katika picha na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Sam Rumanyika kushoto,katika bango linaloonesha namba za kupuga bure kwa ajili ya kutoa taarifa za ukatili mara baada ya uzinduzi wa kipindi hicho uliofanyika jijini Mwanza.picha na Judith Ferdinand
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Sam Rumanyika akizungumza wakati wa uzinduzi wa kipindi cha Konzi la Moyo TV Show kilichoandaliwa na Mwanahabari nguri Florah Magabe uliofanyika jijini Mwanza.picha na Judith Ferdinand
Kamishina Msaidizi wa Polisi,Ofisa Ushirikishwaji Jamii Polisi Mkoa wa Mwanza Hamisi Mwampelwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa kipindi cha Konzi la Moyo TV Show kilichoandaliwa na Mwanahabari nguri Florah Magabe uliofanyika jijini Mwanza.picha na Judith Ferdinand
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Mwakilagi,akizungumza wakati wa uzinduzi wa kipindi cha Konzi la Moyo TV Show kilichoandaliwa na Mwanahabari nguri Florah Magabe uliofanyika jijini Mwanza.picha na Judith Ferdinand
Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Staslaus Mabula,akizungumza wakati wa uzinduzi wa kipindi cha Konzi la Moyo TV Show kilichoandaliwa na Mwanahabari nguri Florah Magabe uliofanyika jijini Mwanza.picha na Judith Ferdinand
Mwandishi Nguri wa habari, Muandaaji wa kipindi cha Konzi la Moyo TV Show Florah Magabe,akizungumza wakati wa uzinduzi wa kipindi hicho ambao umefanywa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Sam Rumanyika, uliofanyika jijini mwanza.picha na Judith Ferdinand
Baadhi ya washiriki waliohudhuria uzinduzi wa kipindi cha Konzi la Moyo TV Show kilichoandaliwa na Mwandishi Nguri wa habari, Florah Magabe,na kuzinduliwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Sam Rumanyika, uliofanyika jijini mwanza.picha na Judith Ferdinand