April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kaimu Katibu Mkuu, Patrick Golwike.

Serikali yatoa maelekezo kwa NacoNgo

Na Zena Mohamed, Timesmajira Online,Dodoma

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imelitaka Baraza la Taifa la mashirika yasiyo ya kiserikali nchini (NacoNgo),kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria taratibu na tamaduni za nchi ili kusaidiana na Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika kujiletea maendeleo.

Hayo yamesemwa jijini hapa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Patrick Golwike wakati wa kukamilisha zoezi la kukamilisha uchaguzi uliofanyika jijini Dodoma.

Amesema kuwa, Baraza hilo linatakiwa kuhakikisha linaweka maslahi ya Taifa mbele na kuhakikisha linasimama badala ya Mashrika yote na sio kwa ajili ya Mashirika machache tu.

Hata hivyo Baraza hilo limetumia mkutano huo kuomba kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ili kuzungumza naye kuhusu mustakabali wa NGOs kwa maendeleo ya Taifa.

Mwenyekiti wa NacoNgo, Liliani Badi.

Akizungumza katika mkutano huo wa kukamilisha zoezi la uchaguzi Mwenyekiti wa NacoNgo, Lilian Badi amesema kuwa, lengo la kutaka kukutana na Rais ni kuweka muelekeo mzuri kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika jitihada za kuhakikisha yanasaidiana na Serikali kuwaletea maendeleo wananchi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali .

“Baraza hili litahakikisha linaleta umoja kati ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini, wadau na Serikali ili kuhakikisha inasaidia utekelezaji wa mipango mikakati iliyowekwa na Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo,”alisema Badi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Dkt. Richard Sambaiga amelipongeza Baraza hilo kwa kuchagua viongozi wake na kuwataka kuwa jicho kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini.

Hayo yote ni Kutokana na hivi karibuni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima kuunda Kamati ya Uratibu wa Uchaguzi wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini (NACONGO) ambao umekamilika kwa kuchagua viongozi wa Baraza hilo kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Taifa.