Na Dixon Busagaga – Kilimanjaro .
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia uwekezaji, Angela Kairuki,ameutaka uongozi wa Kiwanda cha Sukari cha TPC, kilichopo Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, kuangalia uwezekano wa kuanza uzalishaji wa Sukari ya viwandani, ili kuondoa adha ya kuagiza sukari hiyo nje ya nchini.
Kairuki alisema mpaka sasa hakuna mzalishaji wa sukari za viwandani nchini na kwamba serikali huagiza zaidi ya Tani 155,000,na kwamba endapo TPC wataanza uzalishaki huo, watasaidia upatikanaji wa sukari hiyo kwa urahisi.
“Niwashauri TPC, kuangalia ni namna gani,mnaweza kuzalisha sukari za viwandani, tukitambua bado hatuna mzalishaji hata mmoja hapa nchini, ambaye anazalisha sukari za viwandani,tunaagiza zaidi ya tani 155,000 za sukari hii, tunamini mkileta mitambo, mnaweza kuzalisha na kuweza kupata sukari hiyo hapa nchini”alisema Kairuki
Mbali na hilo Kairuki amewataka wawekezaji, kuendelea kutazama fursa za uwekezaji zilizopo nchini na kuwekeza katika nyanja mbalimbali, ili kufanikisha malengo ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda.
Alisema bado kuna mahitaji makubwa ya bidhaa mbalimbali nchini, na bidhaa nyingine zinaagizwa nje ya nchi, hivyo ipo haja kwa wawekezaji kujitokeza na kuwekeza katika nyanja mbalimbali, hatua ambayo itapanua wigo wa ajira kwa watanzania na hata kuinua pato la taifa.
“Mahitaji bado ni makubwa nchini, kuna changamoto ya chupa za kioo,Chupa za Plastiki na bidhaa nyingi tunaagiza nje, sasa angalieni, mkiona kuna fursa, serikali tupo tayari kutoa ushirikiano, ili muweze kupanua wigo wa uwekezaji”alisema Kairuki.
Akizungumza Ofisa mtendaji utawala katika kiwanda cha TPC, Jaffari Ally,alisema mpaka sasa kiwanda hicho kina sukari zaidi ya tani 3,300 ambazo zipo kwenye Ghala, na kuwatoa hofu watanzania, kuwa hakuna tena upungufu wa sukari nchini.
“Tuwatake wasambazaji wakubwa na wauzaji wa rejareja wa sukari nchini, kuacha kuwalangua wananchi na kuhakikisha wanauza sukari kwa bei ya awali ya kabla ya kufungwa kwa msimu, maana kwa sasa sukari inayouzwa inazalishwa hapa nchini na hakuna inayoagizwa nje ya nchi”alisema.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa