July 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yahamasisha wadau kuchangamkia fursa ya cop12

Na.Mwandishi wetu,Timesmajira

SERIKALI imezitaka Wizara, Taasisi za Umma, Sekta Binafsi, Watafiti na Mashirika ya Kiraia kutumia kikamilifu fursa ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), unaotarajiwa kufanyika nchini kuanzia Oktoba 6 hadi 9 mwaka huu.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagilwa, wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu maandalizi ya mkutano huo jijini Tanga Julai 2, 2026.

Kwagilwa amesema Tanzania ilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Mkataba wa Nairobi kwa kipindi cha miaka miwili hadi Desemba 2026 pamoja na kuteuliwa kuwa mwenyeji wa COP12 katika Mkutano wa 11 wa Nchi Wanachama uliofanyika Madagascar mwaka 2024.

Amesema mkutano huo utajadili utekelezaji wa Mpango Kazi wa Mkataba wa Nairobi wa mwaka 2024 hadi 2026 pamoja na masuala mbalimbali yanayohusu uhifadhi na urejeshwaji wa mifumo ikolojia ya bahari ikiwemo mikoko, miamba ya matumbawe na nyasi bahari.

“COP12 ni fursa muhimu kwa Tanzania kuonesha jitihada zake katika usimamizi wa mazingira ya bahari na ukanda wa pwani, huku ikikuza ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika uhifadhi wa rasilimali hizi muhimu,”amesema Kwagilwa.

Amebainisha kuwa Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa sekta ya mazingira na uhifadhi wa rasilimali za maji na bahari ili kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali hizo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha, amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeitambua sekta ya uchumi wa buluu kuwa miongoni mwa sekta za kimkakati zitakazochochea ukuaji wa uchumi, maendeleo ya jamii na uhifadhi wa mazingira.

Kwa mujibu wa Kwagilwa, Tanzania ina fursa kubwa za kunufaika na uchumi wa buluu kupitia sekta za uvuvi, usafirishaji, utalii, nishati, madini na viwanda vinavyotegemea rasilimali za bahari.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, amesema tafiti zinaonesha kuwa mabadiliko ya tabianchi yameanza kuathiri kwa kiwango kikubwa shughuli za uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji mkoani humo.

Amesema utafiti uliofanyika kati ya mwaka 2021 na 2025 umebaini kuwa joto la bahari limeongezeka kutoka nyuzi joto 25.6 mwaka 2021 hadi kufikia nyuzi joto 28.39 mwaka 2024, hali inayochangia mabadiliko ya mifumo ya ikolojia ya bahari.

Dkt. Burian amesema athari hizo zimesababisha kupungua kwa siku za wavuvi kwenda baharini kutoka siku 221 mwaka 2021 hadi siku 170 kutokana na kuongezeka kwa upepo mkali na hatari za usalama baharini.

“Pia mavuno ya samaki yamepungua kwa wastani wa asilimia 25 hadi 30 kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Baraka Luvanda, alisema mkutano wa COP12 unatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki kati ya 500 na 600 kutoka mataifa mbalimbali, wakiwemo viongozi wa serikali, wataalamu wa mazingira na wadau wa maendeleo.

Amesema maandalizi ya mkutano huo yanaendelea kwa lengo la kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na fursa za kiuchumi, kijamii na kimazingira zitakazotokana na tukio hilo la kimataifa.

Mkataba wa Nairobi unahusu hifadhi, usimamizi na uendelezaji wa mazingira ya bahari na ukanda wa pwani wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi, ukiwa unasimamiwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).