May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mhandisi Mwanasha Tumbo akizungumza wakati akifungua kikao cha wajumbe wa Kamati ya Afya ya Msingi Wilaya ya Muheza kulia ni Mganga Mkuu wa Wilaya ya Muheza (DMO) Flora Kessy

Serikali yahamasisha unywaji wa dawa za usubi na minyoo ya tumbo kupitia viongozi wa dini

Na Mwandishi Wetu, Muheza

MKUU wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga Mhandisi Mwanasha Tumbo amewataka viongozi wa dini wa taasisi za serikali na binafsi washirikiana kuwahamasisha jamii na wananchi wakijitokezea kwenye unywaji wa dawa za kutokomeza ugonjwa minyoo ya tumbo na usubi.

Mhandisi Mwanasha amesema wakati akifungua kikao cha wajumbe wa Kamati ya Afya ya Msingi, Wilaya ya Muheza kuwa kumekuwa na fikra potofu kwamba dawa hizo zinazuia uzazi au kusababisha saratani wakati lengo ni kutokomeza ugonjwa wa minyoo ya tumbu na usubi.

Amesema kwa sasa hawatoi dawa za kuzuia na kujikinga na matende kwa sababu yamedhibitiwa kwa kiasi kikubwa na kwamba mafanikio ya kutokomeza ugonjwa wa mabusha yametokana na kufanya operesheni nyingi na kwamba ugonjwa huo umekwisha.

Mwanaisha ametoa wito kwa jamii kama wapo wenye matatizo hayo wajitokeza na kupatiwa matibabu ili kutokomeza kabisa. Amesema kipindi cha nyuma magonjwa ya  matende na usubi, hawayakupewa kipambele, wagonjwa hawakuwa wanafuatilia tiba matokeo yake wakawa wanaambukizana.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Muheza (DMO) Flora Kessy akizungumza wakati wa kikao cha wajumbe wa kamati ya afya ya Msingi kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Muheza Mhandisi Mwanasha Tumbo
Mratibu wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Mkoa wa Tanga Dkt Rehema Maggid akizungumza katrika kikao hicho
Mratibu wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele wilayani Muheza Julias Mgeni akizungumza wakati wa kikao hicho

“Usubri upo hasa kandokando ya mito, mtu anapata ugonjwa wa macho anaona ni ugonjwa wa kawaida lakini hivi sasa wamehakikisha wenye matende wanapata kinga tiba ili kama mtu anapata basi kuhakikisha wadudu hao wanakufa.” Amesema

“Ni muda mrefu wananchi wa Muheza wamekuwa wakipewa dawa ya matende, vipimo vimefanyika na kuonekana ugonjwa huo umekwisha, jitihada hizo tunazielekeza katika usubi.“ amesema Mhandisi Mwanasha

Mkuu huyo wa Wilaya amesema kwa sasa ni kuhakikisha wanajitokeza waliokuwa na wasiokuwa madhara ili kupata kinga ambapo kwa sasa wamebakia asilimia 2.

Hata hivyo amesema kwa upande wa wanafunzi wana sumbuliwa na minyoo na kuna mikakati kuhakikisha wanafunzi wote wanatumia dawa za minyoo ili kudhibiti.

“Lengo la Serikali chini ya Rais Magufuli ni kuhakikisha wananchi wana afya njema ili waweze kuendelea na shughuli za kiuchumi, pia na wanafunzi kusoma kwa bidi. ” Amesema DC.

Naye Mratibu wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele wilayani Muheza, Julius Mgeni amesema wilaya hiyo ilianza kutokumeza magonjwa manne ambayo ni kichocho, usubi, mabusha na matende, minyoo ya tumbo.

Ambapo kwa sasa kiwango cha maambukizi ya mabusha na matende kipo chini ya asilimia 2 hivyo wamesitisha kutoa dawa na badala yake kuelimisha ikiwa ni pamoja na upasuaji mabusha, matende.