Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
SERIKALI imesema inaendelea kuchukua hatua za kupunguza makali ya ongezeko la bei za mafuta nchini, ikiwemo kutoa ruzuku ili kulinda watumiaji na kupunguza athari za gharama za mafuta kwa shughuli za kiuchumi.
Hatua hizo zinalenga kuhakikisha kuwa, pamoja na changamoto zinazoendelea katika soko la dunia, wananchi wanaendelea kupata mafuta kwa uhakika na kwa bei himilivu.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), bei za mafuta nchini zimeongezeka kwa mwezi Novemba 2026 kutokana na kuongezeka kwa gharama za usafirishaji na bima, kulikosababishwa na kuendelea kwa mgogoro wa Mashariki ya Kati, ambako Tanzania huagiza sehemu kubwa ya mafuta yake.
Hali hiyo imejitokeza licha ya bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia kupungua kidogo mwezi Oktoba ikilinganishwa na Septemba 2026.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imefanya jitihada za kuweka ruzuku kwa lengo la kupunguza mzigo wa gharama kwa watumiaji wa mafuta na uchumi kwa ujumla, huku ikiendelea kuchukua hatua za kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa bidhaa hizo nchini.
EWURA imetangaza bei kikomo za mafuta zitakazoanza kutumika Novemba 4, 2026, ambapo kwa Dar es Salaam, petroli itauzwa kwa bei isiyozidi Shilingi 4,083 kwa lita, dizeli Shilingi 4,128 na mafuta ya taa Shilingi 4,117. Licha ya ongezeko hilo, bei za mafuta hayo nchini ziko chini zikilinganishwa na baadhi ya nchi jirani katika ukanda wa Afrika Mashariki (EAC) na zile za Kusini mwa Afrika (SADC).
Pamoja na ongezeko hilo, Serikali imeeleza kuwa itaendelea kufuatilia mwenendo wa soko la mafuta duniani na kuchukua hatua za kupunguza athari zake kwa wananchi na shughuli za uzalishaji, usafirishaji na uchumi kwa ujumla.
Kwa mujibuwa taarifa ya EWURA, kipaumbele cha serikali ni kuhakikisha mafuta yanaendelea kupatikana kwa uhakika nchini, huku gharama zake zikiendelea kuwa himilivu kwa wananchi na uchumi.

More Stories
Serikali yafungua milango ya uwekezaji Sekta ya Nishati
Wanaodaiwa kupanga kufanya fujo hukumu ya Lisu waonywa
Wizara ya Maliasili, Manchester United kuimarisha uhifadhi na utalii