May 10, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoto kupatiwa chanjo ya Surua na Rubella

Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya Nchini imewataka Wazazi, Walezi na Walimu kujitokeza kwa wingi kuwatoa watoto wote kwenye kampeni kubwa ya kupata chanjo ya Magonjwa ya Surua na Rubela ambayo itaanza mwezi wa pili ili kuimarisha kinga zao katika kuepukana na magonjwa ya milipuko.

Akizungumza leo Februari 01, 2024 Jijini Dar es Salaam Wakati wa Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Kutathimini Huduma za Chanjo Nchini kwa mwaka 2023, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amewahimiza wananchi kufanya usafi wa mazingira ili kuendelea kuepukana na magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.

“Ni jukumu la wananchi kujikinga na maradhi ya milipuko kwa kufanya usafi wa mazingira, kunawa mikono ili kuhakikisha wanapoanda chakula katika mazingira bora hasa wakati wa kuwapatia watoto chakula na wazingatie kanuni za Afya” amesema Dkt. Magembe

Aidha, Dkt. Magembe amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kununua vifaa vya afya, hivyo watumishi wanatakiwa kuzingatia maadili katika kuwapa wananchi taarifa sahihi, lengo ni kuhakikisha kwamba wananchi wanahudumiwa vizuri pindi wanapopata changamoto zao kutatuliwa kwa haraka.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amesema takribani mikoa nane tayari ina maambukizi ya kipindupindu, hivyo amewataka waganga wakuu wa mikoa kusimamia afua za usafi ili kuhakikisha miundombinu ya kunawia mikono ipo katika kukabiliana na magonjwa.