May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kasi ujenzi wa mahanga JKT kuchukua vijana wengi zaidi

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Kakonko

KUTOKANA na uwezeshaji unaofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu ,kwa Jeshi la Kujenga Taifa,hivi sasa Jeshi hilo lina uwezo wa kuchukua vijana hadi 50,000 kwa wakati mmoja kutoka vijana 5,000 waliokuwa wakichukuliwa wakati mafunzo ya lazima yanarejeshwa.

 Akizungumza alipotembelea Kikosi cha Jeshi 824 Kanembwa kilichopo wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma,Brigedia Jenerali Mabena amempongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za maendeleo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba miundombinu inakuwa sawa sawa ili kuchukua vijana wengi wa kitanzania kuhudhuria mafunzo ya kundi la lazima (kwa mujibu wa sheria) na kundi la kujitolea. 

Aidha amesema,wakati kiikosi kinaanza baada ya JKT kukabidhiwa kutoka kambi ya wakimbizi , hakikuwa na uwezo wa kuchukua vijana hata 1,000 lakini sasa kikosi kina uwezo wa kuchukua vijana 4000 hadi 5000, huku akisema katika mwaka huu wa fedha unaoishia Juni 30 kikosi hicho kimepewa kiasi cha shilingi bilioni 1.47 kwa ajili ya maendeleo ya kikosi.

“Kwa hiyo kikosi sasa kinajenga mahanga saba ambapo kila hanga moja litachukua vijana 100 kwa hiyo utaona kutakuwa na ongezeko la vijana wengine 700 katika kikosi hiki.”amesema Brigedia Jenerali Mabena

Kwa upande wake Mkurugenzi  wa Fedha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT )Luteni Kanali Eveline Kibisa ameridhishwa na matumjzi ya fedha zinazotumwa katika vikosi vya JKT huku akisema zinafanya kazi iliyokusudiwa na kwa ubora.

Luteni Kanali Kibisa amewapongeza wakuu wa vikosi kwa kujenga majengo mazuri ambayo yana viwango vinavyoridhisha.

Aidha ameishukuru Serikali kwa kuliwezesha JKT fedha za kutosha  hasa katika kipindi cha miaka mitatu ya fedha ambazo zimewezesha karibu kila kikosi kuongeza  mahanga ya vijana na hivyo kuvifanya vikosi kuongeza uwezo wa kuchukua vijana wengi zaidi.

Ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wakuu wa vikosi waendelee kusimamia vizuri pesa wanazoomba kutoka serikalini ili angalau serikali itakavyoona kuna matumizi mazuri ya pesa na wao watapata moyo wa kuendelea kuwasapoti na hivyo kuweza kujenga mahanga mengi zaidi.