May 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuendelea kuboresha vyuo nchini

Na Queen Lema, Timesmajira online, Arusha

Serikali imesema kuwa itaendelea kuboresha mazingira ya ufundi kwa vyuo mbalimbali hapa nchini kwani fani hiyo ni muhimu sana kwa maendeleo ya teknolojia.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Patrobas Katambi wakati akifunga maoneosho ya NACTVET yaliyofanyika katika uwanja wa Stadium mkoani Arusha.

Amesema kuwa mpango huo wa serikali unaenda sanjari na kugusa maeneo mbalimbali ya maendeleo ya vyuo hivyo ikiwa ni pamoja na na kuviboresha ipasavyo.

“Elimu ya ufundi ni moja ya elimu ambayo ni muhimu sana na lengo halisi ni kuona kuwa elimu ya ufundi inapiga hatua ikiwa ni pamoja na kuzalisha mafundi wenye tija,kuepukana na ukosefu wa ajira kwani sekta binafsi inaweza kuajiri watu wengi zaidi,”amesema.

Aidha ametaja mikakati ya serikali katika kumsaidia vyuo kuanzia sasa kuweza kujenga vyuo vya Veta kwa kila Wilaya zote hapa nchini.

Huku mikakati mingine ni pamoja na kuimarisha vyuo vya maendeleo ya jamii hapa nchini ambayo yanalenga kuweza kuongeza kiwango cha ajira.

“NACTVET nayo ipo kwenye mikakati ya serikali yetu kuweza kusaidia kuratibu mipango hiyo ikiwa ni pamoja na kuibua vipaji katika maeneo ya sayansi na teknolojia kwani hilo ni agizo la Rais kuwa kila Wizara ijipange kuzalisha ajira na lengo ni kukuza uchumi wa nchi,”amesema.

Katika hatua nyingine amesema kuwa mpango huo wa vyuo bado haujaweza kuwaacha watu wenye ulemavu kwani nao wana uwezo wa kuchangia maendeleo ya nchi.

“Ukiongelea maendeleo ya vyuo bado tumegusa ambapo serikali imetoa kiasi cha zaidi ya bilioni 2 na mpaka sasa tumeshafungua vyuo zaidi ya 7,”.

Sanjari na hayo amevitaka vyuo mbalimbali kuendelea kubuni aina ya mafunzo ambayo yataweza kuwa chachu katika kuleta mabadiliko ya ajira hapa nchini.

Naye Katibu Mtendaji kutoka NACTVET Dkt. Adolf Rutayuga amesema kuwa wao kama baraza wameweza kufanya maonesho ambayo yamehusisha vyuo mbalimbali.

Huku akitoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanatembelea vyuo mbalimbali ili kupata maelekezo sanjari na elimu ambayo itawasaidia katika kuleta mapinduzi kwenye sekta ya ajira.

khanifa Jonas ni moja ya vijana ambao waliweza kutembelea maonesho hayo katika siku ya kufunga ambapo amesema kuwa NACTVET imeweza kuwafungua macho sana vijana hasa wa Kanda ya Kaskazini kwa kuweza kuwaonesha fursa zilizopo vyuoni.

“Mimi natamani sana kujua jinsi ya kutengeneza bidhaa zenye ubora wa kuaminika na leo nimejionea kutoka katika banda la Arusha Technical ambao pia ni chuo hapo sasa najipanga kujiunga na chuo hicho ila bila haya maonesho nisingeweza kujua au kutambua hilo,”amesema