April 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali Kilimanjaro yazitaka taasisi zenye madeni sugu ya ankra za maji kulipa

Na Martha Fatael,TimesMajira Online,Moshi

SERIKALI mkoani Kilimanjaro imezitaka tasisi zake zenye madeni sugu ya Ankara za maji kuingiza madeni hayo ya zaidi ya sh.bil.3 katika bajeti zao za mwaka ili yamalisize.

Aidha Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA),tayari imeweka utaratibu wa kupunguza madeni hayo kwa kuthibiti kukua kwake kwa kufunga mita za malipo kabla ya matumizi (prepaid).

Mkuu wa mkoa huo, Stephen Kagaigai ameyasema hayo wakati wa ziara yake MUWSA na kutembelea miradi inayosimamiwa na mamlaka hiyo.

Miongoni mwa Taasisi zilizofungiwa mita za Prepaid ni pamoja na Polisi, Magereza na shule ya Polisi Moshi (MPA).

Kagaigai amesema ni vyema wakuu wa taasisi zenye madeni hayo kuingiza fedha wanazodaiwa za ankara za maji kwenye bajeti zao za mwaka ili kumaliza madeni hayo.

Awali katika taarifa yake, kaimu Mkurugenzi wa MUWSA, Mhandisi Kija Limbe amesema mamlaka hiyo inaathiriwa na uwepo wa madeni hayo sugu na kuwa tayari wameweka mkakati wa kuyakabili kwa kufunga prepaid mita.

Amesema mamlaka hiyo inazidai taasisi za Polisi zaidi ya Bil 1.6, shule ya polisi Moshi zaidi ya Bil 1 na magereza zaidi ya mil 400 madeni ambayo yamekuwa yakiongezeka kila mwaka huku wakijadiliana namna ya kuyalipa.

“Tumezungumza nao mara kwa mara kuhusu madeni yao kwani tungepata fedha hizo zingetusaidia kuendelea kuboresha huduma kwa wateja wetu wa eneo la pembezoni lililoongezwa kupata huduma kwenye mamlaka hii” amesema.

Mkurugenzi wa MUWSA, Kija Limbe

Amesema kwa sasa wapo kwenye majadiliano na taasisi hizo ili waingie gharama za usambazaji wa mita hizo ndani ya taasisi zao ili kila nyumba ifungwe mita za kulipia kabla ya kutumia.

Aidha mkurugenzi huyo amesema katika kumaliza tatizo la madeni sugu tayari wamenunua mita za kulipia kabla 443 ambazo thamani yake ni zaidi ya 350,000 kila moja.