Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Mwanza
SERIKALI imeendelea kuthamini mchango unaotolewa na taasisi za kidini nchini katika kuimarisha amani, mshikamano na maendeleo ya taifa.
Hayo yameelezwa Juni 19,2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano Deus Sangu,alipomwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, katika ibada maalum ya kuliombea Taifa la Tanzania katika Kanisa la Kiinjili la Kiluther Tanzania (KKKT),Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria jijini Mwanza.

Akizungumza katika ibada hiyo,Sangu amesema Serikali inatambua mchango muhimu wa taasisi za kidini katika kujenga jamii yenye maadili mema, umoja na mshikamano, mambo ambayo ni msingi wa maendeleo endelevu ya nchi.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote ikiwemo makundi mbalimbali ya kijamii yenye nia njema ya kuijenga Tanzania.
“Tunatambua kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila amani, utulivu, umoja na mshikamano wa wananchi wake,”amesema Sangu.
Sanjari ya hayo amewahasa viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani, upendo, uvumilivu na maadili mema kwa jamii hasa kwa vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa.
Vilevile, amewapongeza Umoja wa Unity of Christian International (UCI) kwa kuweka malengo yanayoendana na Dira ya Taifa 2050 yenye lengo la kujenga jamii yenye mshikamano, upendo, utu na maendeleo.

Kwa upande wake, Askofu Kiongozi Unity Christian International Dar -es-Salaam,Profesa Wilson Munguza, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kushirikiana na taasisi za kidini katika kuimarisha umoja na maendeleo ya taifa.
Ibada hiyo maalum ya kuliombea Taifa viongozi wa dini, waumini na wadau mbalimbali wameshiriki ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuhamasisha amani, umoja na maendeleo ya Tanzania.


More Stories
Kihongosi asimulia magumu aliyopitia, ni kilio na furaha
Sillo:Tanzania itakuwa mwenyeji bora AFCON 2027
ATCL yapanua wigo wa safari