April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Takukuru mkoani Dodoma, Sostenes Kibwengo

Sekta ya Ardhi yatajwa miongoni mwa vinara wa rushwa

Mkuu wa Takukuru mkoani Dodoma, Sostenes Kibwengo

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru ) Mkoani Dodoma, imeitaja sekta ya Ardhi kuwa ni miongoni mwa sekta inayoongoza kwa vitendo vya kupokea rushwa kutoka kwa raia.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Taasisi hiyo Mkoani Dodoma, Sostenes Kibwengo ambaye amesema, hali hiyo imejitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya robo ya pili ya taasisi hiyo na kuonekana sekta hiyo kuwa na asilimia kubwa ya vitendo vya kupokea rushwa kuliko nyingine.

Maeneo mengine yaliyoshika nafasi za juu kwa vitendo vya rushwa ni pamoja na Serikali za Mitaa ambayo ni kwa asilimia 17, Vyama vya Ushirika asilimia 16 pamoja na Sekta ya Walimu ambayo ni asilimia nane.

Pia zipo sekta ya Afya, Ujenzi na Mahakama na zote zikiwa na asilimia saba kwa kila moja huku kwa upande wa Polisi ikiwa asilimia sita.

Kibwengo amewataka watendaji wa sekta hizo kuacha tabia ya kuchukua rushwa kwa sababu Takukuru ipo kila kona kusaka wanaofanya vitendo hivyo.

” Takukuru tunaendelea na uchunguzi katika sekta hizo ambazo zinaendekeza sana mambo ya rushwa dhidi ya utendaji wao na tunawakumbusha viongozi wa maeneo yanayolalamikiwa zaidi hasa yale ambayo ni vinara kwa vitendo vya rushwa mara kwa mara wachukue hatua ya kuboresha mifumo yao ya kufanyia kazi ili kudhibiti vitendo vya rushwa. ” amesisitiza Kibwengo.

Hata hivyo Taasisi hiyo imekamilisha majalada 12 ya uchunguzi na kufungua mashauri 9 mahakamani yaliyowahusisha walimu, wauguzi na watumishi wa halmashauri na kuongeza mashauri manne yalikamilika mahakamani.

Katika hatua nyingine, imemfikisha mahakamani Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi ya Walimu Wilayani Bahi, Adam Richard kwa makosa nane ya kuomba na kupokea rushwa ya sh 450, 000 kutoka kwa walimu wawili ili awasaidie katika mchakato wa kupandishwa madaraja.

Mkuu wa Taasisi hivyo Mkoani Dodoma, Sostenes Kibwengo amesema Kaimu Katibu huyo amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bahi akiwa amefunguliwa shauri la jinai.

Amesema, uchunguzi umeonyesha kuwa mtuhumiwa alitenda kosa kinyume na kifungu cha sheria cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa.