Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
Mfumo wa kufuatilia, kudhibiti na kukusanya taarifa za mafuta yanayoingia nchini kwa wakati halisi (Supervisory Control and Data Acquisition -SCADA) umeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha usimamizi wa mafuta nchini kwa kuongeza uwazi, usahihi wa taarifa na ufanisi katika ushushwaji wa mafuta yanayoingia kupitia bandari zetu hadi kufika kwenye maghala ya kuhifadhia.
Kupitia mfumo huo, Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) umefanikiwa kuimarisha udhibiti wa upotevu wa mafuta na kuongeza uhakika wa takwimu zinazotumika katika kufanya maamuzi ya kiutendaji.
Akizungumza katika mahojiano na gazeti la Uhuru kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, Afisa Lojistiki wa Mafuta wa PBPA, Hilda Kowero, amesema mfumo wa SCADA umeleta maboresho makubwa katika usimamizi wa mafuta kwa kuwezesha ufuatiliaji wa shughuli zote muhimu kwa wakati halisi.

“Teknolojia hii inatuwezesha kupata taarifa sahihi kwa wakati kuhusu mwenendo wa mafuta yanayoingia nchini. Hivyo, tunakuwa na uwezo wa kufuatilia mnyororo mzima kwa usahihi na kuongeza uwajibikaji katika usimamizi wa mafuta,” amesema Kowero.
Ameongeza kuwa pamoja na kuratibu uagizaji wa mafuta kupitia Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (Bulk Procurement System – BPS), PBPA pia ina jukumu la kuhakikisha nchi inakuwa na akiba na upatikanaji wa mafuta unaoaminika wakati wote hivyo kuimarisha usalama wa hali ya upatakinaji wa mafuta nchini.


More Stories
DCEA yawanoa waandishi wa habari kuhusu kemikali bashirifu
CHAKUHAWATA yaiomba serikali kuzuia vikwazo walimu kujiunga Chama chao
Wananchi wawezeshwa kutambua dawa za kulevya Sabasaba