April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Saratani ugonjwa unaosababishwa kwa kugawanyika kwa seli za kiungo chochote

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online

Saratani ni ugonjwa unaosababishwa na kugawanyika kwa seli za kiungo chochote mwilini bila kufuata utaratibu wa kawaida.

Hivyo kusababisha kuzaliwa kwa seli zenye ukubwa,umbo na uwezo wa kufanya kazi tofauti na inavyopaswa na kusababisha dalili hatarishi kwa maisha ya mgonjwa kama vile maumivu,kutoka damu,kidonda kisichopona,uvimbe n.k.

Zipo aina nyingi za saratani kwani kila kiungo cha mwili kinaweza kuwa na saratani mfano Kuna saratani ya matiti,shingo ya kizazi,utumbo mpana,ngozi, ubongo,macho,ulimi,Koo,mapafu,tumbo,in,Figo,kongosho,mifupa,damu n.k.

Daktari Bingwa wa upasuaji Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure, Dkt.Athanas Ngabakubi,amebainisha hayo wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza juu ya namna ya kuandika habari sahihi za afya hususani za ugonjwa wa saratani kupitia mradi Mtambuka wa Saratani Tanzania (TCCP) ambao unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa(AFD) na Aga Khan Foundation (AKF).

Ukubwa wa tatizo la saratani

Dkt.Ngabakubi anaekeza kuwa kwa mwaka 2020 inakadiriwa watu milioni 1.1 walipata saratani,huku watu 711,429 waliofariki kwa saratani Afrika wakati huo Tanzania watu 40,464 walipata saratani kati yao 26,945 walifariki kutokana na saratani.

Dalili ya ugonjwa wa saratani

Dkt Ngabakubi anaeleza kuwa hakuna dalili iliyo maalumu kwa saratani pekee yake hivyo mgonjwa wa magonjwa mengine kama uvimbe,homa,kuchoka sana,maumivu,kutapika,kuharisha,kupungua uzito,vidonda visivyopona,harufu mbaya,kutoka damu ukeni isiyo ya kawaida na nyinginezo.

Anashauri kwamba watu wasisubili kuona dalili yoyote Bali wafanye uchunguzi mapaema wa afya zao ili kubaini kama wana saratani.

Vihatarishi vya saratani

Anaeleza kuwa kuna aina mbili za vihatarishi vinavyoweza kuongeza uwezekano wa mtu kupata saratani ikiwemo vinavyozuilika na visivyoweza kuzuilika.

Hata hivyo anaeleza kuwa moja ya viashiria vinavyoweza kuzuilika ni pamoja na tabia ikiwemo matumizi ya tumbaku,sigara na ugoro,matumizi ya pombe kupita kiasi ambapo kwa siku wanawake na wanaume wasizidi unit 14.

Pia ulaji mbovu usiozingatia lishe bora,uzito uliokithiri,kutokufanya mazoezi,ngono zembe pamoja na mazingira ikiwemo kemikali za viwandani na dawa za kuua wadudu.

Viashiria visivyoweza kuzuilika ni pamoja na jinsi ambapo kuna saratani zinazowapata zaidi wanaume au wanawake.

Historia binafsi ya familia kurithi vinasaba vyenye hitilafu kuwai au kuwa na ndugu aliyewai kupata saratani pia umri ambapo kuna saratani zinazowapata zaidi watoto,vijana au wazee.

Kinga ya ugonjwa wa saratani

Dkt.Ngabakubi, anaeleza kuwa hakuna kinga ya kuzuia mtu asipate kabisa saratani kwenye maisha yake yote lakini mtu anaweza kupunguza uwezekano wa kupata saratani kwa kufanya mambo mbalimbali ikiwemo kupata chanjo kwa saratani zenye chanjo mfano saratani ya ini na shingo ya kizazi.

Pia kubadili tabia hatarishi, kupunguza au kuacha matumizi ya tumbaku na pombe,kuzingatia ulaji unaofaa ikiwemo ulaji wa matunda na mbogamboga,kupunguza ulaji wa vyakula vya mafuta,chumvi,mafuta ya wanyama,nyama nyekundu na vyakula vilivyo sindikwa.

Vilevile kufanya mazoezi angalau mara mbili mpaka tatu kwa wiki, kupunguza uzito,kujikinga na vitu hatarishi kama kemikali, kuzingatia ngono iliosalama,kujikinga na maambukizi ya virusi na bakteria,kujichunguza mabadiliko yasiyo ya kawaida kwenye mwili.

Aidha kuwa na mazoea ya kupima afya na kufanya uchunguzi wa awali mara kwa mara ili ugonjwa ugundulike mapema kwani kuzuia ni bora kuliko tiba.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa magonjwa ya saratani hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Dkt. Beda Likonda,anasema ipo mihimili minne ambayo ikitendewa haki jamii itafikiwa na kuleta matokeo chanya ikiwemo takwimu,elimu,tiba na tiba shufaa

Dkt .Likonda anasema wanatakiwa kutoa elimu kwa jamii,wafanyakazi na wadau wa sekta ya afya,ili wajue saratani ni nini, inatokana na nini,jinsi gani ya kujizuia na je,wafanye nini na wakipata wagonjwa waweze kuwatibu.

Pia anaeleza kuwa serikali inapaswa kuhakikisha tiba zinapatikana kuanzia katika hatua mbalimbali za vituo vya tiba kama vile vituo vya afya, zahanati,hospitali za mikoa na wilaya ili huduma ziwafikie wananchi.

Aidha anasema,mhimili wa nne ni tiba shufaa ambayo mgonjwa anarudi nyumbani hana uwezo wa kumtibu,hata kama atafariki asiwe kwenye matatizo mengi.

“Katika mihimi hiyo ya kupambana na adui yetu saratani,kuna mapungufu mengi,nimefurahi wenzetu wa Aga Khan na Wafaransa wameungana kuona tunaifikia vipi hii mihimili minne,wameanza na mihimili miwili watatusaidia katika kujenga na kuhakikisha mihili yote mine inakamilika ili tuweze kupigana vizuri na saratani (adui yetu),”anasema.

Naye Meneja Ubia,Uwezeshaji na Mawasiliano wa mradi wa TCCP Dkt.Sarah Maongezi anasema, miongoni mwa changamoto katika huduma za saratani nchini hapa ni pamoja na wagonjwa wengi kufika katika hospitali wakiwa katika hatua za mwisho.

Ambapo kubwa zaidi ni uelewa na elimu ndogo katika jamii juu ya saratani huku mradi huo was TCCP unatarajia kuwanufaisha watu milioni 1.7, ikiwemo waandishi wa habari ambao wamewapatia elimu sahihi juu ya saratani hivyo wataweza kufikisha taarifa sahihi kwa jamii kwani inawaamini pia wanauwezo wa kuwafikia watu wengi kwa wakati mmoja.

“Wagonjwa wengi wa saratani wanafika katika hospitali zetu wakiwa katika hatua ya tatu na ya nne,lakini uelewa mdogo katika jamii nina hakika ninyi waandishi wa habari mnajua,pia uhaba wa mashine za tiba ya saratani kuuzwa bei ghali,kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) mashine 1 inapaswa kuhudumia watu milioni Moja na hapa nchini tupo milioni 60 tuna mashine 7 tu,”anasema Dkt.Maongezi.

Daktari Bingwa wa upasuaji Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure, Dkt.Athanas Ngabakubi,akizungumza wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza juu ya namna ya kuandika habari sahihi za afya hususani za ugonjwa wa saratani kupitia mradi Mtambuka wa Saratani Tanzania (TCCP) ambao unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa(AFD) na Aga Khan Foundation (AKF).(picha na Judith Ferdinand)
Meneja Ubia,Uwezeshaji na Mawasiliano wa mradi wa TCCP Dkt.Sarah, akizungumza wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza juu ya namna ya kuandika habari sahihi za afya hususani za ugonjwa wa saratani kupitia mradi Mtambuka wa Saratani Tanzania (TCCP) ambao unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa(AFD) na Aga Khan Foundation (AKF).(picha na Judith Ferdinand)
Baadhi ya Waandishi wa Habari waliohudhuria mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza juu ya namna ya kuandika habari sahihi za afya hususani za ugonjwa wa saratani kupitia mradi Mtambuka wa Saratani Tanzania (TCCP) ambao unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa(AFD) na Aga Khan Foundation (AKF).(picha na Judith Ferdinand)