May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia aanika siri nzito ya Makonda Uenezi CCM

*Asema amekichangamsha Chama, afafanua kulikuwa na uvivu kidogo, kusinzia, ataja sababu ya kumpeleka Arusha, afunda viongozi

Na Jackline Martin,TimesmajiraOnline,Dar

RAIS Samia Suluhu Hassan, ametegua kitendawili na kumteua aliyekuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo Maalum wa CCM, Paul Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, akichukua nafasi ya John Mongella.

Rais Samia ametegua kitendawili hicho, jana Ikulu, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza mara baada ya kuwaapisha viongozi aliowateua kushika nyadhifa mbalimbali.

“Umefanya kazi nzuri CCM, umekichemsha chama kulikuwa kidogo na uvivu uvivu, kila mmoja kutoka hataki, kuna waliosinzia, lakini umekichemsha chama tumeamka vizuri,” alisema Rais Samia na kuongeza;

“Najua ulikuwa RC Dar es Salaam na kwenyewe ulifanya mazuri. Tumekupeleka Arusha, unajua nini kipo huko na unajua nini matumaini yangu kwako huko Arusha.”

Rais Samia amemtaka Makonda aende Arusha akafanye kazi. “Mimi nina imani kubwa nawe na ninaamini utafanya kile ninachotamani ukafanye.”

Rais Samia amesema kubwa Arusha ni utalii, wageni wameongezeka, malazi hakuna kwa hiyo nenda kasimamie ukisaidiana na wawekezaji kuhakikisha wanapata malazi ya kutosha kwa ajili ya wageni (watalii).

“Arusha pia ni mji mkubwa, ni makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na taasisi kubwa zipo kule kwa hiyo nenda kasimamie mkoa uwe na jina zuri,” alisema.

*** Kuhusu uteuzi wa Ndejembi

Akizungumzia uteuzi wa Deogratius Ndejembi, kuwa Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Rais Samia alisema ameamua kumpandisha kutoka kuwa Naibu Waziri wa Tamisemi, kutokana na kazi nzuri aliyoifanya.

“Nimeamua kumpandisha kutoka naibu kuwa waziri kutokanana utendaji kazi nzuri. Kwa hiyo, huko unakokwenda, mbali na kusimamia mifuko, kuna watu wenye ulemavu na vijana, tunatarajia makubwa kutoka kwako.

Wizara yako inasimamia sera ya vijana na watu wenye ulemavu, kazi yako ni kutaribu, ukienda kilimo, kuna vijana, Tmisemi kuna vijana, uvuvi kuna vijana ambao wanategemea sera nzuri ili waweze kufanya mambo yao,” alisema Rais Samia na kuongeza;

Nendeni ukafanye uratibu wa mambo yao. Wizara ya vijana haina kazi kubwa ya kuwa na miradi, kazi kubwa inafanywa na Wizara ya Elimu, lakini baada ya kupata mafunzo wanajiajiri na kuajiriwa, kazi yenu ni kwenda kuratibu.

Kujua wangapi wenye kazi, ni maeneo gani yanatoa kazi, msiangaike kutafuta miradi ya vijana na hivyo hivyo kwa walemavu, kasimamie vyama vya wafanyakazi na kwenyewe nakupa pole kuna kazi kidogo.”

Kuhusu mifuko, alisema hiyo inajiendesha. Alisema hataki kusikia wakigongana na na naibu wake (Katambi) kwani wakigongana wanaondoka wote wawili.

Ripoti ya CAG

Aidha, ameagiza viongozi hao walioapishwa wakafanyie kazi ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, ili hoja zijibiwi na wakizijibu mapema watajua ni wapi bado.

***Zainabu Katimba

Kuhusu Katimba, amesema yeye ndiyo anaingia kwenye unaibu waziri, lakini alimtaka atumie muda mfupi kujifunza na yeye akiwa naibu waziri ndiye atakayekuwa akijibu maswali ya TAMISEMI na anajua ilivyo kubwa.