May 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RUWASA Kilindi wapata bil.4.6 kulipa Wakandarasi

Na Mwandishi Wetu,Kilindi

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga hadi kufikia Machi 30, mwaka huu wameweza kupokea fedha sh. 4,673,195,630 kwa ajili ya malipo kwa Wakandarasi wanaojenga miradi ya maji sawa na asilimia 182 ya bajeti ya wilaya hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ya sh. 2,554,277,528.

Hayo yamesemwa Aprili 29, 2026 na
Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilindi Mhandisi Seleman Mdoe kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.

“Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilindi Mhandisi Seleman Mdoe akizungumza kwenye Baraza”

Mhandisi Mdoe amesema  miradi iliyopelekewa fedha ni ya Diburuma/Songe, Kwamaligwa/Gitu, Kikunde/Ludewa, Kilindi asilia/Misufini na Kilindi asilia/Kwamazuma.

“Katika kuboresha huduma ya maji vijijini katika Wilaya ya Kilindi kwa kipindi cha mwaka 2025/2026, Serikali imepanga kutumia sh. 2,554,277,528 kwa ajili ya ukamilishaji, uboreshsji, utafutaji wa vyanzo na ujenzi wa miradi mbalimbali ya maji katika wilaya yetu, ambapo sh. 903,365,983 ni fedha ya Lipa kwa Matokeo (PforR), sh. 1,150,911, 544 ni fedha za Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF).

“Sh. milioni 500 fedha kutoka Serikali Kuu (GoT) na sh. 20,907,935 ni fedha za matumizi mengineyo (OC), hivyo kufanya jumla ya fedha za bajeti ya RUWASA Wilaya ya Kilindi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kuwa sh. 2,554,277,528. Hadi kufikia Machi 30, 2026 tumepokea sh. 4,673,195,630 kwa ajili ya malipo ya Wakandarasi wanaojenga miradi ya maji, sawa na asilimia 182.96 ya bajeti,”amesema  Mhandisi Mdoe.

“Madiwani wakiwa kwenye kikao cha Baraza.”

Mhandisi Mdoe amesema  katika uendeshsji wa miradi ya maji, Wilaya ya Kilindi ina jumla ya Bodi nane (8) za Usimamizi wa Miradi (CBWOSO’s) zilizoundwa kwa kuzingatia matakwa ya sheria Na.5 ya Maji na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2019.

“Hivyo, miradi yote inayofanya kazi kwa sasa shughuli za usimamizi, uendeshaji na matengenezo madogo madogo, zitafanywa na bodi za usimamizi wa miradi hiyo zilizoundwa. RUWASA itaendelea kutoa mafunzo kwa bodi hizi ili zifanye kazi yake kwa ufanisi na weledi, na kuhakikisha miradi ya maji inakuwa endelevu na kutoa huduma bora kwa wananchi,”amesema Mhandisi Mdoe.

Mhandisi Mdoe amesema  moja ya changamoto inayoikumba miradi ya maji ni kiwango kidogo ama kukatika kwa umeme kunakofanya uzalishaji mdogo wa maji, na ukosefu wa vyanzo vya uhakika vya maji, na baadhi ya visima kuwa na asili ya chumvi.

Amesema mikakati waliyonayo ni uboreshsji wa vyanzo vya maji vilivyopo kwa kupanda miti ili kutunza uoto wa asili uliopo, kuendelea kutafuta vyanzo vya uhakika vya maji ndani na nje ya wilaya hasa Mto Diburuma, na Mto Pangani uliopo Wilaya ya Korogwe, ili kuendana na Sera ya Maji ya mwaka 2002, utekelezaji wa Ilani ya CCM 2025- 2030, na Dira ya Maendeleo ya Serikali ifikapo Desemba 2026 asilimia 85 ya wakazi wa Wilaya ya Kilindi wapate maji safi,salama na ya utoshelevu.

“Wakuu wa Vyombo vya Usalama, Wakuu wa Idara na Vitengo, Afisa Tarafa na waalikwa wakiwa kwenye Baraza.”