August 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

REA yatoa somo la Nishati Safi ya kupikia kwa vitendo Nanenane

Na.Mwandishi wetu,Timesmajira

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Martha Chassama, ameendelea kutoa elimu kwa vitendo kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuandaa na kupika vyakula kwa kutumia majiko ya kisasa yanayotumia nishati safi, ikiwa ni sehemu ya shughuli za uelimishaji wa wananchi wanaotembelea banda la REA katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Akizungumza baada ya onesho hilo, Chassama amesema REA inaendelea kutekeleza kwa kasi miradi ya nishati safi ya kupikia nchini kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa nishati salama, nafuu na rafiki kwa mazingira, sambamba na kuboresha afya za wananchi na kuhifadhi mazingira.

“Nishati safi ya kupikia siyo tu suluhisho la kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, bali ni uwekezaji katika afya za wananchi, uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya uchumi wa familia. REA inaendelea kuhakikisha wananchi wanapata elimu na fursa ya kutumia teknolojia hizi za kisasa ili kuboresha maisha yao,” amesema Chassama.

Amefafanua kuwa maonesho hayo yanatoa fursa kwa wananchi kujionea kwa vitendo namna majiko ya kisasa yanavyofanya kazi, kufahamu manufaa yake pamoja na kupata elimu kuhusu teknolojia mbalimbali za nishati safi ya kupikia zinazotekelezwa na REA kwa kushirikiana na Serikali na wadau wa maendeleo.

Aidha, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia yanachangia kupunguza athari za kiafya zitokanazo na moshi wa kuni na mkaa, kulinda mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti, pamoja na kuokoa muda na gharama zinazotumika katika kutafuta nishati za kupikia.

Chassama amewahimiza wananchi wanaotembelea Maonesho ya Nanenane kutembelea banda la REA ili kupata elimu kuhusu utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, nishati safi ya kupikia na teknolojia za nishati jadidifu, zinazolenga kuboresha maisha ya Watanzania na kuchochea maendeleo endelevu.

Maonesho ya Nanenane ya mwaka 2026 yanaendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, yakitoa jukwaa kwa taasisi za umma na sekta binafsi kuonesha huduma, ubunifu na teknolojia zinazochangia maendeleo ya sekta ya kilimo na uchumi wa Taifa.