December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Tabora aagiza watafiti kuzalisha mbegu bora za alizeti

Na Tiganya Vincent,TimesMajira Online,Tabora

MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani amewaagiza Watafiti kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo –Tumbi cha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania(TARI) kuhakikisha wanazalisha mbegu bora za alizeti zitakazowawezesha wakulima kulima na kupata mavuno mengi.

Hatua hiyo inalenga kuongeza uzalisha wa alizeti kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa mafuta hapa nchini.

Balozi Dkt. Batilda alitoa agizo hilo wakati akipokuwa na ziara ya kikazi katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo –Tumbi cha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania(TARI)

Amesema Nchi inakabiliwa na upungufu mafuta karibu tani laki nne na hivyo jitihada zinahitajika kusaidia kubaini maeneo ambayo yanafaa kwa uzalishaji wa alizeti ili wakulima wapatiwe mbegu bora ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Balozi Dkt. Batilda amesema hatua itasaidia kujua ni ekari ngapi mkoani Tabora zinafaa kwa alizeti na mahitaji halisi ya mbegu bora kwa mashamba yote.

Ameongeza hali hiyo itasaidia kujua Maafisa Ugani wangapi wanahitaji kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kuzalisha kwa ubora na wingi wa zao hilo.

Balozi Dkt. Batilda amesema katika kuhakikisha hilo lifanikiwa ameitisha kikao cha Halmashauri zote na Taasisi zote za Utafiti na wadau wiki ijayo kwa lengo la kupanga mikakati ya kufanikisha zoezi hilo.

Katika Hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora amewapongeza Watafiti wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo –Tumbi cha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania(TARI) kwa kuweza kuzalisha mbegu ya mahindi ambayo umesaidia kuongeza uzalishaji wa mahindi kwa ekari moja hadi kufikia magunia 22.

Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha wananachi wanakuwa na mbegu zitakazowawezesha kuwa na uhakika wa kupata chakula cha kutosha mwaka mzima.

Balozi Dkt. Batilda amewataka Watafiti hao kuongeza pia juhudi katika uzalishaji wa mbegu za viazi lishe na kuzisambaza kwa wananchi ili watu wengi waweze kulima kwa ajili ya kukabiliana na tatizo wa utapia mlo.

Aidha Mkuu wa Mkoa wa Tabora amezitaka kaya tisa zilizovamilia eneo la TARI –Tumbi kuondoka ili waweze kuendelea na shughuli zao za utafiti kwa maslahi mapana ya Nchi.