March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Mgumba: Serikali haitakubali tena ombi la mkandarasi kusogeza mbele muda wa kukamilisha mradi

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online

MKUU wa mkoa wa Tanga Omari Mgumba amesema serikali haitakubali tena ombi la mkandarasi anayejenga mradi wa ujenzi wa gati mbili za kisasa kwenye bandari ya Tanga kusogeza mbele muda wa kukamilisha mradi huo mbali na mwezi novemba aliopewa.

Mgumba ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kwanza katika bandari ya Tanga baada ya Mh Rais kumhamishia Mkoa wa Tanga akitokea Mkoa wa Songwe.

Mgumba amemtaka Meneja wa Bandari hiyo kumsimamia mkandarasi huyo anayetekeleza mradi huo kuhakikisha anaukamilisha kwa wakati uliopangiwa hii ikiwa ni baada ya kuomba kuongezewa muda ili kuukamilisha.

“Maelekezo yangu kwa mkandarasi ilikuwa amalize kazi mwezi wa kumi na atukabidhi lakini ameomba muda tumuongeze mpaka mwezi wa kumi na moja na serikali imemkubalia na baada ya hapo hatutaongeza tena na nimemuomba raisi aje kufungua mradi huu utakapokamilika

Aidha Mgumba amewataka wafanyabiashara wa ndani na nje ya mkoa kuendelea kuitumia Bandari ya Tanga kutuma na kupokea mizigo yao hii ikiwa ni kufuatia mapinduzi makubwa yaliyofanywa na serikali baada ya kuamua kuiboresha hatua ambayo inakwenda kupunguza gharama zilizokuwa ni kikwazo kikubwa kwao.

Mgumba alitoa wito huo kwa wafanyabiashara na wawekezaji baada ya kutembelea na kujionea maendeleo ya mradi wa upanuzi wa kina cha Bandari na upanuzi wa gati ambao umegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 420 unaotarajia kukamilika mwezi November 2022 huku utekelezaji wake ukiwa umefikia asilimia 60 mpaka sasa

Alisema kukamilika kwa mradi huo kutaondoa gharama za kushusha mizigo ambapo awali ilikuwa ni zaidi ya Dola 1 kwa tani na sasa imeondolewa hatua ambayo ni fursa kwa wafanyabiashara na inayokwenda kufungua upya mlango kwao kupelekea mizigo yao ndani na nje ya mipaka ya Tanzania ikiwemo nchi za afrika mashariki.

“Wafanyabiashara wote ambao walikuwa na hofu au walikimbia kuitumia Bandari hii ya Tanga kutokana na gharama kubwa hapo nyuma sasa hivi hiyo ni historia na tumeiondoa kutoka Dola 1 kwa tani haipo tena sasa hivi ni sifuri gharama zimepungua kwahiyo hii Sasa Bandari ndio yenye gharama mdogo kuliko zote hapa nchini na Afrika Mashariki” alisema .

“Bandari ya Tanga ina mchango mkubwa kwa Maendeleo ya mkoa na hata taifa kwa ujumla mwaka huu katika Bandari hii shehena imeongezeka ikitofautishwa na miaka ya nyuma na hii imetokana na uwekezaji mkubwa wa serikali yetu ya awamu ya sita inayoongozwa na raisi wetu leo matunda yanaanza kurudi ambapo tukimaliza mradi huu matunda yataonekana zaidi kwahiyo mapato kwa wananchi na uchumi wa taifa letu utaongezeka zaidi” alisema Mgumba.

Aidha Mgumba alisema kuwa kutokana na changamoto ya uhaba wa upanuzi wa maghala ya kuhifadhia shehena ameitaka mamalaka zingine zinazomiliki maeneo hayo kuyarudisha kwenye milki ya Bandari ili kuangalia namna bora ya kuongeza maghala huku akiwataka wawekezaji kuitumia fursa hiyo ambayo itakuwa ni fursa kwao kupata soko kwa ukanda wa Afrika Mashariki.

“Changamoto kubwa niliyoibaini ni kwamba bandari wana uhaba wa maghala ya kuhifadhia shehena hii kubwa , sasa serikali tutaongea mamalaka nyingine wakiwemo TBA ili tuone namna bora ya kuwarudishia hayo maeneo yaweza kuwasaidia kuhifadhia shehena kubwa” alisema Mgumba.

Akizungumza meneja wa bandari hiyo Masoud Mrisha alisema kuwa mpaka sasa mradi huo umeshafika asilimia 60 za utekelezaji na uwezo wao ni kuhudumia tani laki 7 , 17400 kwa sasa na mara baada ya kukamilika aatakuwa na uwezo wa kuhudumia shehena ya tani million 3 hatua ambayo inakwenda kuufungua mkoa na kuiongezea mapato Bandari hiyo na serikali kwa ujumla.

“Mradi wetu umefikia asilimia 60 za utekelezaji uwezo wetu kwa Sasa ni kuhudumia tani laki 7,17400 na utakapokamilika tutaweza kuhudumia tani million 3 pamoja na meli zenye urefu wa mita 220 mbili zitaweza kukaa kwa pamoja na kuzihudumia ni matarajio yetu kwamba ifikapo mwezi november shughuli zote za utekelezaji wa mradi zitakuwa zimekamilika ” alisema Mrisha.

Mradi huo unaotekelezwa na mamalaka hiyo serikali iliwekeza zaidi ya shilingi Bilioni 420 kwaajili ya upanuzi wa kina cha Bandari chenye urefu wa mita 450 ambao upo awamu ya pili ya utekelezaji pamoja na ujenzi wa gati hatua ambayo kukamilika kwake itaweza kupokea meli kubwa za nje ya nchi ikiwemo nchi za Afrika Mashariki zitakazokuja kushusha na kupokea mizigo .