December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Makalla: Hakuna tena mgao wa maji Dar

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amosi Makala amesema kuwa mgao wa maji uliokuwa unaendelea katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani hautakwepo tena kufuatia kuongezeka kwa maji kwenye chanzo cha Mto Ruvu ikiwa ni matokeo ya mvua zinazoendelea kunyesha kwenye mikoa mbalimbali.

Ametoa tamko hilo wakati akiwa kwenye ziara ya kutembelea na kujionea hali ya upatikanaji wa maji kwenye chanzo hicho baada ya kupungua kwa maji kwa miezi kadhaa kulikosababishwa na hali ya ukame.

Amesema kuwa kwa sasa mgao wa maji kwa Dar es Salaam na Pwani sasa basi, huduma imerejea kama kawaida na kuwataka wananchi kuendelea kutunza mazingira pamoja na kuhifadhi vyanzo vya maji ili huduma ya maji iendelee kupatikana.

“Nimetembelea na nimejionea hali ya maji katika chanzo cha maji cha Ruvu Chini maji yamerejea katika hali yake na yapo ya kutosha,” ameeleza Mhe Makala.

Ameongeza kuwa jitihada za wazi zilifanyika na Serikali za kuhakikisha huduma ya maji inarejea katika hali yake ikiwemo kukabiliana na uharibifu wa vyanzo vya maji kwa kuwaondoa wavamizi kwenye vyanzo vya maji vinavyoleta maji kwenye Mto Ruvu.

“Nipende kumshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano wake alioutoa wa kuwezesha mradi wa maji Kigamboni kwa kutoa fedha bilioni 23 zilizowezesha kukamilika kwa mradi na kuweza kuhudumia wananchi wa maeneo ya katikati mwa Jiji kupata maji kupitia mradi huo, kiasi cha lita milioni 70 kiliingizwa mjini na kusaidia kuhudumia wananchi wa maeneo ya katikati mwa jiji,” ameeleza.

Mhe. Makala ameiagiza DAWASA kuhakikisha huduma imaimarika kwa kuwezesha miundombinu yote ya maji iliyopo inatoa maji ili kila mwananchi apate maji kikamilifu.

“Naomba DAWASA mrudi kazini na mhakikishe miundombinu ya maji inaimarishwa na inatoa maji kikamilifu ili wananchi wote wapate maji kwa kuwa mgao sasa umeisha,” amesisitiza.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kuwa kwa mara ya kwanza sasa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani umekuwa na maji mengi na ya ziada yanayowezesha kukidhi mahitaji ya maji.

Ameongeza kuwa kufuatia kukamilika kwa mradi wa maji Kigamboni kumeongeza kiasi cha lita milioni 70 za maji mjini na kuongeza uzalishaji kufikia lita milioni 590 kutoka uzalishaji wa awali wa lita milioni 520 za maji kwa siku, hivyo kupitia uzalishaji wa lita milioni 590 tunaweza kukidhi mahitaji ya maji ya lita milioni 544 kwa siku.

“Tunaishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kutuwezesha kuvuka kwenye kipindi hiki kwa kusukuma ukamilishwaji wa mradi wa maji Kigamboni, lakini pia kupitia visima virefu vilivyoboreshwa na kuingizwa kwenye mfumo ambavyo jumla vimezalisha lita milioni 33.1, kazi yote hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza makali ya maji,” ameeleza Mhandisi Luhemeja.

Mhandisi Luhemeja amesisitiza wananchi kuendelea kutunza mazingira na vyanzo vya maji kwa kuepuka uharibifu wa vyanzo vya maji ili huduma iendelee kupatikana.