May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yahimiza uhsirikiano wawadau katika utekelezaji wa PJT-MMMAM

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

SHIRIKA lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na mapambano dhidi ya maambukizi ya virus vya UKIMWI hasa kutokomeza ukimwi kwa watoto la Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation limezindua mradi wa Malezi awamu ya tatu uliolenga kusaidia utelezaji wa Programu Jumuishi ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) ya 2021/22-2025/26.

Tanzania ina watoto na watu wazima milioni 1.7 wanaoishi na virus vya ukimwi (VVU) ambapo mwaka 2019 kulikuwa na maambukizi mapya ya virus hivyo 77,000 nchini (makadirio ya VVU ya UNAIDS 2020).

 Akizungumza katika uzinduzi huo jijini Dodoma Kamishna wa Ustawi wa Jamii,Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum  Dkt.Nandela Mhando alihimiza uhusiano wa kati ya EGPAF na Serikali  ili  kuchangia kwenye jitihada za kutoa huduma za Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) na kuhakikisha watoto wote nchini wanakua katika muelekeo sahihi wa kufikia ukuaji timilifu.

 “Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwenu, hivyo  nasi tutahitaji ushirikiano wenu bega kwa bega katika utekelezaji wa Malezi awamu ya tatu ,nan i matumaini yangu  kwamba taarifa za utekelezaji wa mradi huu zitaingia katika mfumo mpya wa  taarifa wa serikali.”amesema Dkt.Nandela na kuongeza kuwa

 “Serikali inategemea  kwamba ,huduma mtakazotoa za MMMAM zitahakikisha watoto wote nchini wanakuwa kwenye muelekeo sahihi wa kufikia ukuaji timilifu,hili ni jambo muhimu sana kwa sababu mnafahamu tuliyonayo sasa hivi ya kuwa na watoto wa mitaani na changamoto kwenye masuala ya MMMAM ili wazazi waweze kuwa karibu na watoto wao.”

Mkurugenzi wa Mtandao wa Malezi na Makuzi (TECDEN)  Mwajuma Rwebangila

Aidha ametumia nafasi hiyo kuwataka Maafisa Ustawi wa Jamii nchini  kufanya utambuzi wa watoto wote watakaobainika kuwa ni changamoto ili waunganishwe na huduma mtambuka wakati wa utekelezaji wa mradi huo wa Malezi III.

Awali Mwakilishi wa  Mkurugezi Mkurugenzi Mkazi wa EGPAF  Dkt.Charles Mkoko amesema,Shirika hilo linalojishughulisha na mapambano dhidi ya maambukizi ya Virus vya UKIMWI hasa kutokomeza UKIMWI kwa watoto .

Amesema,kwa kutambua umuhimu wa MMMAM shirika limekuwa likifanya kazi kwa kushirikiana na wizara ya Maendeleo ya Jamii na wizara ya afya katika kutekeleza miradi ya MMMAM na kwamba Shirika limekuwa liktekeleza mradi wa MMMAM kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano yaani Malezi awamu ya kwanza na Malezi awamu ya pili  katika mkoa wa Tabora.kwa kipindi cha miaka mitano kwa awamu mbili tofauti kuanzia 2015 hadi 2020.

Kwa mujibu wa Mkoko  Mradi  wa Malezi awamu ya kwanza na Malezi Awamu ya pili umekuwa mstari wa mbele kuisaidia Serikali katika kuongeza uelewa wa MMMAM pamoja na kujumuisha huduma za MMMAM katika sera na miongozo ya kitaifa ikiwemo uanzishwaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya MALEZI,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) na uboreshaji wa kifurushi cha ufuatiliai wa mtoto chini ya miaka mitano.

“Pamoja na mambo mengine,katika utekelezaji wa miradi hiyo miwili tumefanikiwa kuanzisha kona za uchangamshi zilizochorwa na kuwezeshwa na vifaa vya michezo kulingana na umri katika vituo vya afya 86 mkoani Tabora “amesema

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo Mradi wa Malezi awamu ya tatu utatekelezwa katika mikoa ya Tabora na Arusha ukilenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana chini ya miradi ya Malezi awamu ya kwanza na ya pili na kufanikisha uendelevu wa kujumuisha huduma za MMMAM na mifumo ya afya katika ngazi ya Taifa na Mikoa.

Mkurugenzi wa Mtandao wa Malezi na Makuzi (TECDEN)  Mwajuma Rwebangila

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mtandao wa Malezi na Makuzi (TECDEN)  Mwajuma Rwebagila amesema,pamoja na mafanikio ambayo yameendelea kuonekana katika utekelezaji wa PJT- MMMAM ambapo wadau wameanzisha miradi mbalimbali ya watoto lakini bado kuna pengo la kufikisha elimu hiyo kwenye ngazi ya Jamii.

“Kwa hiyo kupitia hadhira hii ningeomba hawa wadau kwa kuwa wana watu wanaofanya nao kazi kule chini wakafikishe ujumbe wa MMMAM  kwenye ngazi za familia,kwenye ngazi za jamii ,hilo ni  ombwe ambalo tumekuwa tukiliona kila tunapokutana na wadau wengi sana ,wanaonyesha hilo pengo haswa katika kufikisha elimu ya MMMAM kwenye ngazi ya jamii na tukifanya hivyo tutakuwa na uwezo wa kurekebisha zile nyendo ambazo tunaziona Taifa linakoelekea siyo hususan kwenye masuala ya ulinzi na usalama wa mtoto.”amesema Rwebangila