Na Mwandishi wetu,timesmajira,Online
Rais Samia Suluhu Hassan, amezindua Mkakati wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Akizungumza kabla ya kuzindua Mkakati huo, Rais Samia amesema Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika mwaka 2022 ina lengo la kufahamu idadi ya watu, mahali walipo, jinsia, rika, elimu, ajira, shughuli, makazi yao, mahali yalipo na hali yake.
Rais Samia amesema taarifa hizo zitasaidia kufahamu wastani wa ongezeko la idadi ya watu katika nchi na pia hali ya uhamiaji kutoka vijijini kwenda mijini na kuwezesha nchi kutambua hatua mbalimbali za kimaendeleo.
Aidha, amesema Sensa inasaidia Serikali kufanya maamuzi kuhusu ugawaji wa rasilimali za Taifa na kupeleka huduma mbalimbali za jamii kwa wananchi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu kwenye maeneo yao kulingana na idadi ya watu na mahitaji.
Amesema mbali na kupitia madodoso ya Sensa ya mwaka 2022, Sensa hiyo itawezesha kutambua idadi ya majengo na mahali yalipo, itawezesha kufahamu hali ya mahitaji ya makazi nchini na kufahamu na kupanga mitaa kupitia anuani za makazi ambazo zitachochea benki kutoa mikopo na kupunguza viwango vya riba.
“Naomba viongozi wa Serikali, Dini na vyama vya siasa  kusisitiza wananchi kushiriki kikamilifu kwenye zoezi hilo la Sensa ya Watu na Makazi,nawasihi viongozi Dini msisahau kuzungumzia suala la Sensa kila mnapokuwa mkitoa mahubiri kwa waumini wenu,”amesema
Rais Samia ameishukuru na kuipongeza Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa kwa kukamilisha mkakati wa Uelimishaji na Uhamasishaji Sensa mapema na kuwataka kwenda kuutekeleza.
Tukio hilo la uzinduzi limehudhuriwa pia na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Dkt. Khalid Salim Mohamed, Mawaziri, Manaibu Mawaziri, viongozi wa Dini pamoja na vyama vya siasa.
More Stories
TMDA:Toeni taarifa za ufuatiliaji usalama wa vifaa tiba ,vitendanishi
The Desk & Chair yashusha neema Gereza la Butimba
TVLA,yapongezwa kwa kuzalisha chanjo