April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia awataka watetezi wa haki za binadamu kutobagua makundi ya kutetea

Na Penina Malundo ,timesmajira,Online

RAIS   Samia Suluhu Hassan amewataka Watetezi wa haki za binadamu nchini,kutetea kweli haki za binadamu ,  kuhimiza watu kufanyakazi kwa bidii na uwajibikaji ili  haki hizo  za binadamu zionekana kwa uwazi.

Rais Samia ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya miaka 10 ya Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),amesema watetezi hao wanapaswa kutotetea haki za  kisiasa bali watetee makundi ya watoto katika jamii ikiwemo wale wanaobakwa.

Amesema kuwa kazi ya kulinda haki ya mwanadamu inapaswa kufanywa na watu  wote ili kuwaletea wananchi maendeleo kwa sababu haki ya binadamu ni maendeleo na maendeleo ni kitovu kwa wanadamu.

“Kuheshimu haki za binadamu ni sehemu ya maendeleo ya nchi na Tanzania imekua na sera ya maendeleo iliyozingatia haki ya mwanadamu tangu mwaka 1967 tulipotangaza azimio la Arusha,”amesema  na kuongeza

“Dhana nzima ya watetezi wa haki za binadamu mimi kama mwanadamu pia nakubaliana nayo,”amesisitiza

Amesema kutokana na matakwa ya tamko la umoja wa mataifa la watetezi wa haki za binadamu la 1998 na ibara ya 8 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania serikali ina jukumu na ni mtetezi mkuu wa kulinda haki za kijamii haki za binadamu na haki za watu.

“Mtetezi mkubwa wa haki za binadamu ndani ya Tanzania ni katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo serikali ndio inatekeleza ndio sheria mama ambayo ina haki zote za wanadamu wanaoishi Tanzania,”amesema 

Kwa upande wake Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa amesema wamezindua  taarifa yao ambayo itaweka wazi kwa miaka 10 wamefanya nini na wanatarajia kufanya nini kwa miaka ijayo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo kutoka kwa Mwenyekiti wa THRDC Jaji Mstaafu Joaquine De Mello kutokana na mchango wake wa kulinda na kusimamia haki za binadamu na utawala wa Sheria katika kipindi cha mwaka mmoja tangu aingie madarakani.