January 2, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia atuma salamu za pole kifo cha Waziri Kwandikwa

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Venance Mabeyo, kufuatia kifo cha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Elias John Kwandikwa kilichotokea  tarehe 02 Agosti, 2021 Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais Samia amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mhe. Kwandikwa ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ushetu mkoani Shinyanga kutokana na mchango wake mkubwa katika utumishi wa umma.

“Tumempoteza mtu muhimu ambaye mchango wake katika utumishi wa umma hautasahaulika, Kwandikwa alikuwa kiongozi shupavu ambaye alikuwa akitekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na taratibu”. Amesema Mhe. Rais Samia.

Mhe. Rais Samia amemtaka Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo kufikisha salamu zake za pole kwa familia ya Marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na watu wote walioguswa na msiba huo.

Bwana ametoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe, Amina.

Jaffar Haniu

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.