May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaipongeza OSHA kujali wenye ulemavu

Na Bakari Lulela,TimesMajira Online

SERIKALI imesisitiza kwamba itaendelea kufanya jitihada mbalimbali katika kuwajumuisha watu wenya ulemavu katika nyanja zote za uchumi na kutoa wito kwa wadau kutoa mchango wao katika kuliwezesha kundi hilo hususan watoto wadogo ili waweze kupata elimu na malezi bora yatakayowawezesha kutimiza ndoto zao na hatimae kutoa mchango wao katika maendeleo ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, Ummy Nderiananga alipokuwa akikabidhi vifaa mbalimbali vya msaada katika shule za watu wenye ulemavu ambavyo vimetolewa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa kazi (OSHA) ikishirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Amesema watoto wenye ulemavu wana uwezo mkubwa ambao hutofautiana na watu wasiokuwa na ulemavu hivyo endapo watalelewa vizuri na kupata stahiki wanaweza kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.

“Niwashukuru OSHA kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kufanya ziara katika shule tatu za watoto wenye ulemavu OSHA imekuwa ni taasisi ya faraja sana kwa watu wenye ulemavu kwani katika kile kidogo wanachokipata wakashirikiana nami na Ofisi nzima ya Waziri Mkuu kuja kuwatembelea hawa watoto. Hivyo binafsi nimefarijika sana,” amesema Naibu Waziri huyo wa Nchini anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu na kuongeza

“Natamani kuona watu wenye ulemavu wanajumuishwa ipasavyo katika sekta zote na ndio maana nimekuwa nikipita katika maeneo mbalimbali ikiwemo ajira ,elimu, afya, uchumi ili kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanapata nafasi katika kila fursa inayotokea na katika mipango mbalimbali ya serikali.

Mtendaji Mkuu wa wakala wa Usalama na Afya Mahala pa kazi (OSHA) Khadija Mwenda (mwenye kiremba chekundu) akishiriki zoezi la kugawa chakula kwa wanafinzi wa shule ya msingi Buigiri wasioona ambacho kiliandaliwa sambamba na msaada wa vifaa mbalimbali vilivyokabidhiwa katika shule hiyo na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (watu wenye Ulemavu) mhe. Ummy Nderiananga. Viongozi hao walishiriki chakula hicho pamoja na wanafunzi, walimu na watumishi wengine wa shule hiyo.

Aidha, Naibu Waziri huyo amesema serikali itaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo zikiwemo Taasisi ,Asasi zisizo za kiserikali, makampuni na watu binafsi katika kuwawezesha watu wenye ulemavu ili nao waweze kutoa mchango wao katika kuijenga nchi yao.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa kazi (OSHA).

OSHA ambao ndio wameandaa vifaa hivyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu amesema msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Taasisi yake wa kusaidia jamii kwenye sekta za elimu, afya, majanga na uboreshaji wa mazingira ya kazi.

“Sisi tumekuja katika shule hizi za watu wenye ulemavu kwa ajili ya kutoa faraja kwa wanafunzi na watumishi wenzetu ambao wanafanyakazi katika mazingira yenye changamoto nyingi na vihatarishi vingi vikiwemo vihatarishi vya kisaikolojia hivyo wanahitaji kutiwa moyo ili waendelee kuifanya kazi hii ambayo kimsingi ni kazi kubwa na muhimu sana katika maendeleo ya Taifa letu,”amesema Mtendaji Mkuu wa OSHA.

Aidha,wanafunzi na Viongozi wa baadhi ya shule zilizopatiwa msaada wa vifaa hivyo. wameishukuru taasisi ya OSHA kwa msaada uliotolewa na kuwaomba wadau wengine kuendelea kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazozikumba shule za watoto wenye ulemavu.

“Binafsi nimefarijika sana kwa sababu sikujua kuwa OSHA watakuja kwani walinipigia tu simu wakiniuliza changamoto tulizonazo hivyo namshukuru sana Naibu Waziri Ummy ambaye kwa kushirikiana na OSHA wameona waje watutembelee na kutuletea zawadi.

“Kiukweli mahitaji waliyotuletea ni ya muhimu sana kwetu hatujawahi kuwa nayo tangu shule hii ilipoanzishwa kwa mfano wametuletea vifaa vya kuzimia moto na kompyuta ambayo itatusaidia sana katika kuandaa mitihani ya wanafunzi,” amesema Kajika Gallani mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mazinyungu.

Msaada huo wenye thamani takribani milioni 15 ulihusisha ukaguzi wa usalama na afya hususan katika mabweni ya wanafunzi umetolewa katika shule za msingi za watoto wenye Ulemavu za Uhuru mchanganyiko za Ilala Dar es Salaam, Mazinyungu ya Kilosa Morogoro na Buigiri ya Chamwino Dodoma.

miongoni mwa vifaa vilivyotolewa ni pamoja na kompyuta, vifaa vya kuzimia moto, taulo za kike, vifaa kinga, vifaa vya usafi, karatasi na vibao maalumu vya kuandikia watu wenye ulemavu.