May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia apeleka Kaliua bil. 23.6/- za maendeleo

Na Allan Vicent, TimesmajiraOnline, Kaliua

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora imepokea zaidi ya sh bil 23.6 kutoka Serikali Kuu katika mwaka wa fedha 2023/2024 ili kufanikisha utekelezaji shughuli mbalimbali za maendeleo ya wananchi.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Japhael Lufungij, alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji shughuli za maendeleo kwenye kikao cha baraza la madiwani katika kipindi cha miezi 3 kuanzia Okt-Des 2023.

Amesema kuwa fedha hizo zimesimamiwa na kutumika ipasavyo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kulipa mishahara ya watumishi wa idara mbalimbali.

Amebainisha kuwa kiasi hicho ambacho ni sawa na asilimia 56.8 ya bajeti yote ya halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ya sh bil 41.6, kimewezesha Wataalamu wa idara mbalimbali kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

‘Tunamshukuru sana Rais kwa kutuletea zaidi ya bil 23 kwa ajili ya utekelezaji shughuli za maendeleo ya wananchi ikiwemo kukamilisha baadhi ya miradi ambayo utekelezaji wake ulikuwa unasua sua kwa muda mrefu’, alieleza.

Aidha alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Jerry Mwaga na Wataalamu wake kwa kukusanya zaidi ya sh bil 4.7 za mapato ya ndani ambazo ni sawa na asilimia 99.8 ya makisio yake kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Lufunguja amesisitiza kuwa katika robo ya kwanza tu kuanzia Oktoba hadi Desemba 2023 halmashauri imetumia zaidi ya sh bil 2.2 za mapato yake kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya elimu na afya ili kupunguza kero miongoni mwa jamii.

Ametaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa kuwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa sekondari ya Makingi, jengo la utawala katika shule ya sekondari Jerry Mwaga na uendelezaji wa bwalo la chakula katika shule ya sekondari Kazaroho.

Mingine ni ukamilishaji miundombinu katika Vituo vya Afya Ilege, Uyowa, Igagala, Ukumbisiganga na zahanati za Makonge, Wachawaseme na Igombe na ukamilishaji miundombinu ya sekondari ya Usenye, Konanne na jengo la maabara.

Lufungija alibainisha miradi mingine iliyotekelezwa kwa fedha hizo zikiwemo zilizoletwa na Rais kuwa ni ununuzi wa mashine ya kufua umeme (generator) ya hospitali ya wilaya na ujenzi wa shule mpya za sekondari katika kata za Usinge (Ugansa), Igagala, Kasungu, Ushokola (Makubi), Ulyankulu (Ikonongo na Kaswa.

Aidha halmashauri ilijenga matundu ya vyoo katika shule za msingi Mpwaga, Mpandamlowoka na Kazana Upate pia imeendeleza ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi wa halmashauri na kupeleka fedha katika miradi mingine iliyopangwa kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha.