May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mpango aridhishwa usambazaji gesi asilia

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

MAKAMU wa Rais Dkt.Philip Mpango ameoneshwa kuridhishwa na kazi inayofanywa na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) ya kuwaunganishia wananchi gesi asilia kutoka kwenye bomba kuu.

Akizungumza wakati wa kukagua mabanda kwenye Kongamano la Wanawake la Nishati safi ya kupikia, Dkt.Mpango amesema shirika hilo linafanya kazi nzuri ambayo itachangia wananchi kuachana na nishati chafu ya kupikia.

Hata hivyo amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo  Mussa Makame kuhakikisha wanaendelea kusambaza gesiasilia kwa wananchi huku akilitaka shirika hilo liangalie uwezekano wa njia za kulipatia pesa shirika kwa ajili kuliongezea nguvu katika utekelezaji wa majukumu yake.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC  Makame  amesema shirika hilo limeanza safari ya
kuwezesha wananchi wa Mikoa ya Lindi,Mtwara,Pwani na Dar es Salaam kutumia gesi asilia inayozalishwa hapa nchini.

Aidha amesema mpaka sasa  wameshaunganisha takriban taasisi 13 zikiwemo baadhi ya magereza na shule pia wameunganisha wananchi 1500.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo amesema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni usambazaji wa gesi kwa bomba njia ambayo gharama yake ni kubwa huku akisema wanaangalia uwezekano wa kusambaza gesi asilia kwa njia ya mitungi ili kuwezesha wananchi wengi zaidi kuhama kwenye matumizi ya kuni na mkaa na badala yake waanze kutumia nishati safi ya kupikia.