May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia amaliza kilio cha wafanyakazi Urafiki

Na Penina Malundo

RAIS Samia Suluhu Hassan, amehitimisha kilio cha miaka 10 cha wafanyakazi wa Kiwanda cha Nguo Urafiki baada ya Serikali kutoa kiasi cha sh. bilioni 2.4 kwa ajili ya kuwalipa madai hayo.

Kufuatia uamuzi Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO kama Taasisi iliyosajiliwa na Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri Tanzania, kimeishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia, kwa kuwapatia ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya shughuli zao za chama na kuwasaidia kufanikiwa kulipa wafanyakazi hao.

Tangu uamuzi wa kutaka wafanyakazi hao kulipwa miaka 10 iliyopita, malipo ya wafanyakazi hayo yalishindikana na sasa malipo hayo yamekuja kufanyika chini ya uongozi wake.

Mbali na Serikali kutoa fedha hizo, TUICO imeanza rasmi kuhakiki majina ya wanachama hao kwa lengo la kuanza kuwaingizia fedha zao, ambapo madai yanayohusiana na posho za kodi ya nyumba, usafiri na chakula ambayo yalianza tangu mwaka 2008 hadi 2013.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TUICO, Boniphace Nkakatisi, alisema chama chao kimekuwa na mafanikio makubwa, katika kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sekta kuu nne walizonazo ambazo ni Sekta ya Viwanda, Sekta ya Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri.

“Tunaishukuru Serikali kwa ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya shughuli zetu za Chama na kwa jitihada zinazoonekana wazi, wazi katika kuhakikisha wafanyakazi wanastahili kupata haki zao kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini na Sheria ya Utumishi wa Umma, sambamba na Sheria Bunge nyingine mbalimbali, Katiba na Kanuni za Chama chetu,’’amesema na kuongeza

“Tunayofuraha kubwa sana kwa Chama kufanikisha kumaliza Mgogoro wa Muda mrefu baina ya wafanyakazi wa Kiwanda cha Nguo Urafiki dhidi ya Mwajiri wao na Serikali, ambapo Machi 24, 2023,Chama kilifanikiwa kusaini mkataba wa kumaliza mgogoro uliokuwa mbele ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi yaani Ukazaji Deni Tuzo Namba. 164/2021 ambao ulitokana na Mgogoro wa Marejeo Namba 58/2019,’’amesema.

Amesema Serikali imeweza kutekeleza kwa vitendo kulipa madeni ya madai ya wafanyakazi nchini na kuheshimu vyema maamuzi ya Mahakama pale ambapo wafanyakazi wameshinda mashauri yao dhidi ya Serikali.

“Chama kinaahidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa Serikali, waajiri wote, vyama vya wafanyakazi na Chama cha Waajiri katika kutekeleza shughuli za Chama kwa nia njema ili haki na maslahi ya wafanyakazi nchini na kuheshimika kwa mikataba ya hali bora iliyopo iendelee kusimamiwa vyema na Wafanyakazi,’’amesema.

Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa TUICO,Noel Nchimbi, alisema katika kipindi cha Januari mpaka Septemba, 2023, Chama imefanikiwa kushughulikia jumla ya migogoro ya kazi 301 ikiwemo ya ngazi ya ana kwa ana ambapo chama kilipokea migogoro 42 na kufanikiwa kusuluhisha migogoro 41 na unaondelea ni mgogoro mmoja,

Pia amesema chama kilishughulikia migogoro ya ngazi ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ambapo chama kilipokea migogoro 134 ambapo imefanikiwa kumaliza kwa kufanikiwa migogoro 60 na inayoendelea katika hatua za usuluhishi na uamuzi ni Migogoro 74.

‘’Kuna migogoro tuliyoshugulikia kwa ngazi ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ambapo Chama kilipokea migogoro 125 ambapo tumefanikiwa kumaliza kwa mafanikio migogoro 108 huku inayoendelea ni migogoro 15.

“Katika kipindi cha Januari mpaka Septemba, 2023 hatukuweza kufanikiwa jumla ya migogoro 2 na inayoendelea mpaka sasa ni jumla ya migogoro 90 ambayo tunaamini kwa umakini na wataalam tulionao katika Chama, tutafanikiwa katika kipindi cha mwaka 2024,’’amesema na kuongeza