May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Makamba awataka Nordic kuwekeza kwa vijana wa Afrika

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba amezitaka nchi za Nordic kutumia fursa za ushirikiano zilizoko kati yao na Afrika kuwekeza kwenye nguvu-kazi ya Afrika kwani ndio Bara lenye idadi kubwa ya vijana tofauti na Ulaya.

Ameyasema hayo akichangia hoja katika ufunguzi wa Kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nordic na Afrika (Nordic-Africa Foreign Ministers Meeting) jijini Copenhagen, Dernmark, akiongeza kuwa mwitikio mkubwa wa mwaliko wa ushiriki wa viongozi wa Afrika ni ushahidi tosha wa matamanio ya kukuza ushirikiano wenye tija kati ya Nordic na Afrika.

Waziri Makamba ameongeza akuwa vijana wengi wa Afrika wamekuwa wakihama makazi ili kutafuta kazi Ulaya mbali na vikwazo mbalimbali wanavyokutana navyo na suluhusho la kudumu ni kuwekeza kwa hawa vijana waweze kujiendeleza wakiwa nyumbani.

“Kutakuwa na shida ya wahamiaji hapo baadaye [Nchi za Nordic]. Ni vyema kuhakikisha kuwa vijana wanapata maarifa na ujuzi wa kuwasaidia huko walipo lakini pia hapo baadaye wanaweza kuja na kusaidia katika maendeleo ya nchi za Nordic kutokana na ujuzi mliowapatia,” amesema Waziri Makamba.

Hoja hiyo imeungwa mkono na viongozi wengine wa Afrika wakizitaka nchi za Nordic kuwekeza Afrika ili kupunguza usafirishwaji wa malighafi kwenda nje na kurudishwa kama bidhaa zinazoenda kuuzwa kwa gharama kubwa zaidi, yenye kukandamiza wazalishaji.

Wamesisitiza kuwa umuhimu wa uhusiano wowote unatokana na mchango wa uhusiano huo katika kukua kwa pande zote mbili. Huku wakisisitiza kuwepo kwa msimamo usiobadilika katika kutekeleza yale wanayokubaliana bila ya kulegeza msimamo huo kwa baadhi ya nchi.