April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia ahimiza Mahakama kutenda haki kwa wakati, azionya zisiwaumize wanyonge

Na Zena Mohamed,Timesmajira OnlineDodoma

RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan ameagiza Mahakama kupunguza mlolongo wa muda wa kesi za madai ili wananchi wapate haki kwa wakati.

Amesema hayo jijini Dodoma wakati akihutubia wananchi kwenye kilele cha Siku ya Sheria nchini ambayo yamefanyika katika viwanja vya Chinangali.

Amesema kuchelewa kutoa haki kunapelekea watu wengi kupoteza haki zao au kuchelewa kuzipata jambo ambalo linaweza kumalizwa kwa wakati.

“Kwenye mahakama za chini kesi za madai zinakwenda hadi miezi 12 na Mahakama za Rufani hadi miezi 24, hii siyo sawa kabisa ni lazima tubadilike sasa ili watu wetu wapate haki stahiki na kwa wakati,” ameagiza Rais Samia.

Hata hivyo amesema kazi ya kutoa haki ni ya Mungu mwenyewe kwa hiyo waliopewa dhamana watende kwa haki waepuka kuwaumiza wanyonge.

Amesema iliwalazimu kuanzisha huduma za kisheria kwa wanachi wasio na uwezo kupitia Mama Samia Legal Aid Campaign kutokana na malalamiko kuwa mengi kwani kila pembe kuna malalamiko.

“Tuliona kama Serikali kuna umuhimu wa kuanza na kampeni hii, lakini tunashukuru imetekelezwa vizuri kwa wananchi na niseme kamapeni hiyo inaendelea vizuri na kwa jinsi ilivyopokelewa ni wazi kuwa kuna uhitaji wa msaada wa kisheria hapa nchini,”amesema

Ameeleza kuwa hadi sasa tayari kampeni hiyo imefikia wanachi 383,293 katika mikoa sita, Dodoma, Manyara, Shinyanga, Ruvuma, Singida na Simiyu ambapo kupitia kampeni hiyo migogoro 511 ilitatuliwa na imesaidia nchi kubaini migogoro mingi kwenye jamii.

Ametaja maeneo yawaliyoyabaini kuwa na shida zaidi ni ardhi, matunzo ya watoto, ndoa, mirathi, ukatili wa kijinsia.

Kutokana nakubainika kwa hayo, ameitaka Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na wadau kutekeleza kikamilifu utoaji wa msaada wa kisheria kwa mujibu wa sheria.

“Hivyo wale wote wanaoguswa na haki za jamii tunaomba wajitokeze kufanya jitihada hizi hapa tunawekeza kupatikana kwa haki.

Mheshimiwa Jaji Mkuu, umesema Ushirikiano katika kujitathmini umebaini mapungufu yetu katika taasisi zetu, nami nakuunga mkono kwenye hilo kama ulivyofanya kwa REPOA, hivyo taasisi zingine zote tushirikiane kubaini mapungufu kwa pamoja ili kurekebisha mapungufu,” amesisitiza Rais Samia.

Vile vile amesistiza kuharakishwa kusikilizwa kwa kesi za biashara, ambapo amesema wanapovutia mitaji na uwekezaji nchini na kufungua fursa za kibiashara wanatambua kwamba uwekezaji unaambatana na masuala ya kisheria na migogoro ya kibishara ni vyema kwa mahakama zetu zitoe umuhimu kwa mashauri ya namna hiyo pia.

“Mheshimiwa jaji Mkuu Ibara ya 107 kifungu (a) kifungo kidogo cha pili a mpaka (e) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kimeweka kanuni za kuzingatia pindi Mahakama inapotoa uamuzi wa mashauri mbalimbali.

Kanuni hizo ni kutenda haki kwa wote bila kujali hali ya mtu ya kijamii na kiuchumi kutochelewesha haki bila sababu ya msingi, kuukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro na kutenda haki bila kufungwa kupitia kiasi au kasi ya masharti ya kiufundi yanayoweza kukwamishwa kutenda haki,”amesema.

Amefafanua kuwa unapochukua hatua za usuluhishi unaharakisha kupatikana kwa haki na haileti chungu na maovu.

“Unajua hukumu inaleta chungu na maovu kwa yule anayehukumiwa kwa yule ambaye haki haiendi upande wake, lakini usuluhishi wote wanakubaliana kwa hiyo inaondosha machungu na maovu.

Kwa hiyo ningeomba sana kwamba tuifuate ibara ile ambayo nimeiosoma ambayo ina mambo manne,moja likiwa ni kutenda haki kwa wote,kutochelewesha haki,kutofunga na masharti yakiufundi kupitia au kupita kiasi na kutoa kipaumbele katika usuluhishi,” amesema.