April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia aandika historia, akutana na kufanya mazungumzo na Papa Francis Vatican

RAIS Samia ameandika historia kwa kukutana na Kiongozi Mkuu wa Kanisa Kanitoli Duniani, Papa Francis, ambapo viongozi hao walikuwa na mazungumzo yao ya faragha yaliyodumu kwa takribani dakika 25.

Aidha, viongozi hao wameridhika na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Tanzania, mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu hususan katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii pamoja na changamoto ambazo Tanzania inapitia kwa sasa.

Baadaye, viongozi hao walijielekeza zaidi katika masuala ya kijamii, kikanda, kimataifa na umuhimu amani.

Aidha Rais Samia akipokea zawadi kutoka kwa Baba Mtakatifu Francis, ikiwa ni takribani miaka 17 tangu Rais Mstaafu Jakaya Kikwete wa Tanzania alipotembelea mjini Vatican na kukutana na Baba Mtakatifu Benedikto XVI tarehe 19 Januari 2012.

Katika mazungumzo ya dakika kumi na tano, viongozi hawa wawili waligusia kuhusu: Majadiliano ya kidini, amani katika eneo la Maziwa Makuu, Afya, Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ni katika muktadha wa kujenga na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican, jana Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.

Baadaye, Rais Samia alikutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa.

Rais Samia Suluhu Hassan katika ziara hii ya kitaifa, alikuwa ameambatana na Mama Evaline Malisa Ntenga, ambaye hivi karibuni amechaguliwa kuwa ni Mjumbe wa Bodi Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani na Rais wa WUCWO Afrika, ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAWATA, Taifa, nchini Tanzania.

Wengine ni Prof. Deogratias Rutatora, Mwenyekiti Halmashauri ya walei, Taifa; Leonard Mapolu, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Wakatoliki Wafanyakazi Tanzania, Taifa, VIWAWA; Dalmas Gregory, Mwenyekiti Halmashauri Walei, Jimbo Katoliki la Zanzibar pamoja na Theresia Seda, Mwenyekiti wa Utoto Mtakatifu, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican ulianzishwa kunako tarehe 19 Aprili 1968 na Askofu mkuu Pierluigi Sartorelli akateuliwa kuwa ni Balozi wa kwanza wa Vatican nchini Tanzania, utume alioutekeleza hadi tarehe 22 Desemba 1970.

Uhusiano huu kama alivyobainisha Baba Mtakatifu Benedikto XVI wakati akipokea hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Ali Abeid Aman Karume wa Tanzania mjini Vatican unasimikwa katika tunu msingi za Amani, haki, mshikamano na uhuru, kwani haya ni mambo yanayopata asili yake kutoka katika utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Daima ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yakipewa msukumo wa pekee.

Tangu mwanzo wa mchakato wa uinjilishaji nchini Tanzania, Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi hususan katika nyanja za elimu, afya, maendeleo na ustawi wa jamii, bila kusahau huduma ya maisha ya kiroho kwa watu wa Mungu nchini Tanzania na katika mchakato wa kudumisha amani ulimwenguni.

Takwimu zinaonesha kwamba, Kanisa Katoliki nchini Tanzania linamiliki na kuendesha shule za awali 240, shule za msingi 147, shule za sekondari 244, vyuo vya ufundi, vyuo vikuu 5; taasisi za elimu ya 5 na vituo vya vyuo vikuu 2 ambavyo viko chini ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino, SAUT.

Vyuo vyote hivi vina jumla ya wanafunzi 31, 000 pamoja na taasisi za afya ni 473, lengo likiwa ni kumhudumia mtu mzima kiroho na kimwili.